• HABARI MPYA

    Friday, June 26, 2015

    TAIFA STARS YAINGIA KAMBINI BAGAMOYO, MAZOEZI DAR

    Kocha Mkuu Stars, Charles Boniface Mkwasa
    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeingia kambini jana jioni katika hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani Pwani, lakini leo asubuhi imefanya mazoezi Uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam.
    Kocha mpya wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ juzi alitaja kikosi cha wachezaji 26 kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza kuwania tiketi ya kucheza michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2016 dhidi ya Uganda wiki ijayo mjini Kampala.
    Mkwasa, ambaye alimteua gwiji Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ kuwa Mshauri wake wa Ufundi, jana alifanya kikao na wachezaji wote katika hoteli ya Tansoma, Gerezani, Dar es Salaam kabla ya kwenda nao kambini.
    Kikao cha jana, Mkwasa aliwaelimisha wachezaji juu ya uzalendo kwa taifa lao na umuhimu wao baada ya kuteuliwa kuwa wachezaji wa timu ya taifa.
    Wachezaji 26 walioingia kambini jana kuanza maandalizi ya kwenda kupindua kipigo cha 3-0 wiki mbili zijazo mjini Kampala, Uganda ili kusonga mbele CHAN ni makipa; Mudathir Khamis (KMKM), Mwadini Ali (Azam FC) na Ally Mustafa ‘Barthez’ (Yanga) na mabeki ni Shomary Kapombe (Azam), Michael Aidan (Ruvu Shooting), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba SC), Mwinyi Hajji Mngwali (KMKM), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga SC), Kevin Yondan (Yanga SC), Hassan Isihaka (Simba SC), Aggrey Morris (Azam FC).
    Viungo ni Jonas Mkude (Simba SC), Abdi Banda (Simba SC), Salum Telelea (Yanga SC), Frank Domayo (Azam FC), Simon Msuva (Yanga SC), Said Ndemla (Simba SC), Ramadhani Singano ‘Messi’ (Simba SC) na Deus Kaseke (Mbeya City).
    Washambuliaji ni John Bocco (Azam FC), Atupele Green (Kagera Sugar), Rashid Mandawa (Kagera Sugar), Ame Ali (Mtibwa Sugar), wakati wengine ambao wamewekwa akiba ni Juma Abdul wa Yanga SC, Mudathir Yahya wa Azam FC na Samuel Kamuntu wa JKT Ruvu.
    Mara baada ya kuteuliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kurithi mikoba ya Mholanzi, Mart Nooij aliyefukuzwa mwishoni mwa wiki kufuataia kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Uganda katika mchezo wa kwanza na Uganda, Mkwasa alitaja benchi lake Ufundi, akimteua King Kibaden kuwa Mshauri wake wa Ufundi.
    Hemed Morocco kocha Msaidizi, Manyika Peter kocha wa makipa, Mtunza Vifaa ni Hussein Swedi ‘Gaga’, Meneja Juma Mgunda na Mratibu Msafiri Mgoyi, wakati Daktari atatajwa baadaye.
    Stars itaendelea kuwa kambini Kiromo na kufanya mazoezi Boko Veterani hadi itakaposafiri kwenda Uganda.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS YAINGIA KAMBINI BAGAMOYO, MAZOEZI DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top