• HABARI MPYA

    Sunday, June 28, 2015

    HUO USWAHIBA WA TFF NA YANGA UNAODUMAZA SOKA YA TANZANIA, YETU MACHO!

    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), linamiliki Uwanja mmoja tu wa michezo, Karume uliopo kwenye ofisi zake eneo la Ilala, Dar e Salaam.
    Ni Uwanja mdogo na maalum kwa mazoezi tu, ambao pia haukidhi mahitaji ya kuitwa kituo cha mazoezi ya kisasa ya timu, lakini angalau upo.
    Uwanja wa Karume ni maalum kwa mazoezi ya timu za taifa zote, wanawake na wanaume kuanzia vijana hadi wakubwa.
    Uwanja huo pia hutumika kwa programu za mafunzo ya uwanjani ya marefa, makocha na kadhalika.
    Binafsi, nitaukumbuka zaidi Uwanja huo ambao zamani ulitumika kwa michezo ya Ligi mbalimbali nchini, namna ulivyosaidia kuendeleza vipaji vya vijana kadhaa, ambao kwa sasa ni tegemeo la taifa kama Thomas Ulimwengu na Himid Mao.
    Vijana hao wawili baada ya kuibuliwa kupitia mashindano ya Copa Coca Cola, waliingizwa kwenye kituo cha soka nchini, TSA kilichokuwa mali ya TFF hatimaye leo ni wachezaji wakubwa.
    Si kila anayepita La Masia, akademi ya Barcelona basi atakuwa mchezaji mkubwa baadaye- vivyo hivyo hata vijana wa TSA si wote waliendelea kisoka, wengine wamepotea.
    Lakini hatuwezi kuacha kujivunia Ulimwengu anayechezea TP Mazembe ya DRC na Himid Mao wa Azam FC ya nyumbani Tanzania.
    Katikati TSA ilikufa, lakini siku za karibuni TFF ikaanza mchakato wa kuifufua na tayari mafunzo kwa vijana wadogo yalikuwa yakifanyika kila mwishoni mwa wiki pale Karume.
    Kwa Dar ez Salaam pekee, tunahitaji angalau Karume tano ili kupanua wigo wa uendelezaji w vipaji- hatimaye siku moja tuje kuwa na wachezaji wengi waliokulia katika misingi ya soka.
    Tunafanya mashindano mengi ya vijana wadogo ya kuibua vipaji- mwisho wa siku tunawaendelezaje? Hilo ni swali ambalo nimekuwa nikiuliza mara kadhaa na majibu ni hakuna.
    Klabu nchini zinatakiwa kuwekeza katika soka ya vijana, lakini ukiondoa Azam FC ni klabu nyingine ipi Tanzania ina akademi?
    Wakati hali halisi ni kwamba Karume tu haitoshelezi kwa mahitaji ya programu za timu za taifa pekee, ajabu sasa TFF imeiruhusu klabu ya Yanga kuufanya huo kuwa Uwanja wao wa kudumu wa mazoezi.
    Tangu mwishoni mwa msimu uliopita, Yanga SC wamekuwa wakipatikana Uwanja wa Karume kwa programu zao zote za mazoezi, sasa je timu za taifa ziende wapi?
    Wiki iliyopita nilisikitishwa mno na kuikuta Yanga SC ikifanya mazoezi Uwanja wa Karume chini ya makocha wake, Mholanzi, Hans van der Pluijm na mzalendo Charles Boniface Mkwasa, huku timu mbili za taifa za wanawake, U20 na ya wakubwa, Twiga Stars zikigalagala katika vumbi na kocha wao Rogasian Kaijage.
    U20 wanajiandaa na mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia, wakati Twiga wanajiandaa na fainali za Michezo ya Afrika- lakini wote kwa sasa hawawezi kutekeleza programu zao kisa Yanga SC.
    Ile timu ya vijana chini ya umri wa miaka 13 inayoandaliwa kucheza fainali za U17 mwaka 2019 ambazo tutakuwa wenyeji, ilikuwa Dar es Salaam wiki iliyopita kabla ya kwenda Mbeya, ilikuwa inafanya mazoezi wapi ikiwa Yanga wameuhodhi Karume?     
    Nafahamu Rais wa TFF, Jamal Malinzi ni mwanachama wa Yanga na amewahi kuwa Katibu wa klabu hiyo mwanzoni mwa karne hii ya 21, lakini sitaki kuamini kama nguvu zake zimewapa jeuri hiyo Yanga SC.
    Aidha, sote tunafahamu agizo la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutaka klabu zote zinazoshiriki mashindano ya Afrika kuwasilisha jina la Uwanja wake rasmi wa mazoezi.
    Na CAF imesema klabu ambayo haitakuwa na Uwanja wa mazoezi kuanzia mwakani, haitashiriki michuano ya Afrika.
    Azam FC ambao watacheza Kombe la Shirikisho mwakani wana Uwanja ambao hadi CAF inautambua, hawana presha- ndugu zetu Yanga SC ambao watacheza Ligi ya Mabingwa Uwanja wao ni upi?
    Na bahati mbaya zaidi kwa kulemazwa na TFF kuachwa watumie Uwanja wa Karume, wamesahau kufanya jitihada za kuwa na Uwanja wao rasmi wa mazoezi.
    Sahau kuhusu yote hayo, tunazungumzia maendeleo ya soka ya Tanzania na klabu nchini zinatakiwa kuwekeza katika soka ya vijana- ikiwa TFF inazisaidia zisiwe na viwanja vyake maalum vya mazoezi, matokeo yake ni nini?
    Hiyo ni nchi ambayo soka yake imeporomoka kiasi cha kusikitisha na tayari wengi kati ya wananchi wake wamejiridhisha tatizo ni hakuna wachezaji- kumbe pia hakuna hata jitihada za kutengeneza wachezaji.
    Siku zote najiuliza Yanga SC wanashindwa nini kuwa na Uwanja wao- ikiwa maeneo makubwa lukuki na mazuri yapo kibao Dar es Salaam pekee na klabu ina uwezo wa kutosha.
    Mjumbe mmoja tu wa Kamati ya Utendaji ya Yanga SC, (Isaac Chanji) ana uwezo wa kuifanya siku moja tu klabu hiyo iwe na eneo lake kubwa la kuwekeza Uwanja wa mazoezi.
    Lakini Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji ya Yanga SC wana uwezo mkubwa kifedha, bahati mbaya fedha zao zinaishia kununua wachezaji wa kigeni kwa gharama kubwa, timu haina Uwanja wa mazoezi tu.
    Hayo ni matatizo yao Yanga SC tuwaachie wenyewe, lakini hili la programu za timu za taifa kusimama kupisha mazoezi ya Yanga SC Uwanja wa Karume ni kosa.
    Yanga wana Mwenyekiti tajiri Yussuf Manji aliyesaidia dola za Kimarekani 500,000 Umoja wa Afrika- wanashindwaje kuwa na Uwanja wao hadi ‘wamilikishwe’ Karume, huku programu za timu za taifa zikisimama?
    Kama ni uswahiba wa TFF na Yanga SC unaruhusu kudumaza soka ya Tanzania, basi yetu macho! Ramadhan Karim.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HUO USWAHIBA WA TFF NA YANGA UNAODUMAZA SOKA YA TANZANIA, YETU MACHO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top