• HABARI MPYA

  Jumanne, Juni 23, 2015

  FC VITO WAENDA FINLAND KUSHIRIKI HELSINKI CUP, MALINZI KUWAAGA IJUMAA DAR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, Ijumaa wiki hii anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa hafla ya kuiaga timu ya FC Vito Kilwa ya Kilwa mkoani Lindi, ambayo Jumamosi itasafiri kwenda Finland kushiriki michuano ya Helsinki Cup 2015.
  Akizungumza na mwandishi wetu, Mkurugenzi wa Sports Development Aid (SDA), Chigogolo Mohamed, alisema hafla hiyo itafanyika Ubalozi wa Finland nchini, ulioko makutano ya mitaa ya Garden na Mirambo katikati ya jiji la Dar es Salaam.

  Chigogolo alibainisha kuwa, washiriki katika hafla hiyo ni pamoja na Maofisa kutoka Ubalozi wa Finland, wachezaji wa timu ya vijana ya FC Vito Kilwa, wawakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Wizara ya Michezo na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
  Wataalamu kutoka SDA yenye Makao Makuu mjini Lindi na LiiKe Finland ya Helsinki nchini Finland, wanahabari, na wengineo watahudhuria hafla ya hiyo maalum ya kuwaaga vijana hao 12 chini ya miaka 11 wanaokwenda kushiriki michuano hiyo.
  Chigogolo aliwataja vijana watakaoagwa na kusafiri kushiriki michuano hiyo inayoanza Julai 5 hadi 10 jijini Helsinki kuwa ni Charles Fulco, Hussein Bandari, Hussein Hassani, Shabani Mpogolo, Rashidi Masimba, Hassani Salum na Yahaya Ruambo.
  Wengine ni pamoja na Alex Muhando, Shabani Kikali, Twahili Ismail, Alafat Babu na Ahmad Kokolo, ambao watakuwa chini ya kocha Mohamed Mtule, huku Chigogolo mwenyewe akiwa ni Mkuu wa Msafara (HOD). Timu itatua Dar kesho Alhamisi.
  FC Vito Kilwa ni timu ya tatu kutoka mkoani Lindi, kushiriki michuano ya Helsinki Cup, ambayo ni michuano ya nne kwa ukubwa barani Ulaya miongoni mwa michuano ya vijana, ikihusisha zaidi ya timu za vijana 1,200 toka pande mbalimbali duniani.
  Timu hiyo inamilikiwa na taasisi mbili zisizo za Kiserikali (NGO’s) za SDA na Liike Finland, inawasili Dar es Salaam Alhamisi ikiwa na vijana wa kiume 12 walio na umri chini ya miaka 11 na wataondoka Jumamosi kwenda Helsinki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: FC VITO WAENDA FINLAND KUSHIRIKI HELSINKI CUP, MALINZI KUWAAGA IJUMAA DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top