• HABARI MPYA

  Monday, December 01, 2014

  WASANII WA TAARAB WANATENGANISHWA NA MSTARI MWEMBAMBA KATI YA UKWELI NA UNAFIKI

  MBUNGE mmoja majuzi pale mjengoni alisema kuna watu wana “Ashk Majnun” ya kutaka ukubwa akimaansiha wana ‘wazimu’ au hamu iliyopitiliza ya kutaka ukubwa. Na mimi pia nachukua fursa hii kusema kuwa kuna wasanii wa taarab wana ashk majnun ya kuudharaulisha muziki wa taarab.
  Ukiondoa muziki wa kizazi kipya (Bongo Fleva) ambao unatawala kwa zaidi ya masaa 20 katika vituo vingi vya radio kila siku iendayo kwa mungu, muziki wa taarab ndiyo unaopeta zaidi kuliko aina nyingine ya muziki iliyobakia.
  Uchunguzi unaonyesha zaidi ya asilimia 80 ya vituo vya radio, vina vipindi vya taarab vya masaa matatu kila siku, achilia mbali vituo vichache vyenye vipindi vya lisaa limoja. Hali iko hivyo hivyo kwenye vituo vya televisheni, taarab imetengewa takriban lisaa limoja kila wiki katika vipindi vya ambavyo hurudiwa mara mbili au tatu kwa wiki.

  Hali kama hiyo haipo kwenye muziki wa dansi, ukianza kuhesabu dakika za muziki wa dansi kwenye vituo vya radio au televisheni, utabaki ukistaajabu ni wapi unaelekea muziki huo ambao ulikuwa kijogoo kwa karne nzima iliyopita.
  Hiyo ndiyo bahati ya muziki wa taraab ambao kwa sasa umekuwa kipenzi cha watu wote – wake kwa waume, wakubwa kwa wadogo …muziki ambao hapo awali ulikuwa unaonekana kama vile ni muziki wa kike.
  Ilifika wakati mwanaume ukipenda taarab lazima watu wakutazame kwa jicho la tatu. Lakini leo dhana hiyo imepotea japo baadhi ya wasanii wanalazimisha dhana hiyo irejee.
  Wasanii wa taarab (japo si wote) wanaishi kwa unafiki, wanakunywa unafiki, wanakula unafiki, wanaoga unafiki – wanatenganishwa na mstari mwembamba sana kati ya unafiki na ukweli.
  Inafika wakati unashindwa kabisa kuamini kauli ya msanii wa taarab, leo atasifia kazi ya msanii mwenzake kwako lakini kesho atakashifu kazi hiyo hiyo kwa mtu mwingine. Msanii huyu anabisha hodi kwa mtangazaji wa radio kukabidhi kazi yake, kesho msanii mwingine anampigia simu mtangazaji kuiponda kazi hiyo. Anaibuka mwimbaji mpya, mwimbaji mkongwe anafanya hila, anaibuka mtunzi chipukizi, mtunzi mzoefu anafanya hila, msanii chipukizi naye pia anajazwa ujinga wa kuwadharau waliomtangulia.
  Kwa bahati nzuri ofisi inayonipatia ugali wangu wa kila siku, inanikutanisha na wasanii na wadau wa muziki wa kila aina, napata kila aina ya gumzo kuhusu wasanii na niseme wazi kuwa wasanii wa taraab wanakulana nyama wenyewe kwa wenyewe, hakuna wasanii waliojaa unafiki kama wasanii wa taarab.
  Kutokana na ushindani wa vipindi vya taarab ulivyo, kila mtangazaji anajaribu kupiga wimbo utakaokidhi viwango na utakaoteka wasikilizaji bila kujali jina la msanii wa bendi. Ushindani huo pia umefanya watangazaji wengi wakwepe kabisa kitu kinaitwa rushwa, neema ilioje hiyo kwa muziki wa taarab?
  Kipindi cha taarab kina masaa matatu, muda unaotosha kupigwa nyimbo nyingi kadri iwezekanavyo. Hivi unapokwenda kupiga fitna kwa mtangazaji ili kazi ya mwenzako isipigwe matarajio yako ni nini? Kipindi kizima kipige nyimbo zako au za bendi yako? Ujinga ulioje huo.
  Unapoikashifu nyimbo au kazi ya mwenzako unakuwa unailinganisha na kazi ipi? Ya kwako au ya wasanii wengine? Wakati mwingine ukimskia msanii wa taarab anavyokashifu nyimbo za wenzake halafu ukaitathmini kazi yake utajikuta ukiamini kuwa baadhi ya wasanii wa taarab ni “Ashk Majnun” wa unafiki, ni watu wenye hamu ya unafiki katika kila sekunde ya maisha yao ya kila siku.
  Ukitazama matusi wanayopena wadau wa taarab kwenye mitandao ya kijamii, utagundua kuwa nao ni Ashk Majnun” wa unafiki, wanatumwa kukaanga mbuyu huku wala hawajui ni yupi mwenye meno wa kuutafuna.
  Kwa mfumo wa maisha wanaokwenda nao wasanii wa taarab ni wazi kuwa itafika wakati watawalazimisha watangazaji wenye akili za kushikiwa kugawanyika kwa matabaka ya unafiki, mashabiki watagawanyika kwa matabaka yaliyojaa chuki na matusi na mwisho wa siku kila mtu ataudharau muziki wa taarab.
  Ukibahatika kuonyeshwa picha (screenshot) za mijadala ya wasanii wa taarab na wadau wao kupitia whatsapp, au ukibahatika kusikiliza sauti za wasanii wa taarab zilizorekodiwa kupitia maongezi ya simu na kushuhudia namna wanavyokulana nyama, utabaki ukijisemea: “Masikini wasanii wa taarab, hawajui walifanyalo”.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WASANII WA TAARAB WANATENGANISHWA NA MSTARI MWEMBAMBA KATI YA UKWELI NA UNAFIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top