• HABARI MPYA

  Tuesday, December 02, 2014

  LIGI YA TANZANIA BORA KULIKO YA KENYA, ASEMA IMBEM WA COASTAL ALIYETOKEA KPL

  Na Vincent Malouda, NAIROBI
  MSHAMBULIAJI wa zamani wa AFC Leopards na Gor Mahia, Itubu Imbem ambaye kwa sasa anacheza Coastal Union ya Tanzania, amesema kwamba Ligi ya Tanzania ina ushindani zaidi ya Ligi Kuu ya Kenya, KPL.
  Imbem alichezea klabu za Kenya, Tusker FC, AFC Leopards na Gor Mahia kabla ya kwenda Al Hilal ya Yemen na baadaye kujiunga na Coastal Union, ambayo kwa sasa inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa pointi zake 11.
  Wakati Ligi ya Tanzania, VPL ikiwa imesimama kwa sasa hadi baadaye mwezi huu, mchezaji huyo ameisifu kwamba ni bora kiushindani kuliko ligi ya Kenya.
  Itubu Imbem amesema Ligi ya Tanzania ni ngumu kuliko ya Kenya

  “Nimecheza ligi zote na ninaweza kusema ya Tanzania ni ligi moja yenye ushindani zaidi kutokana na timu zote zinazoshiriki kuwa nzuri,”amesema mshambuliaji huyo wa Wagosi wa Kaya.  
  “Kwa Kenya kuna mwanya mkubwa kati ya timu bora na klabu nyingine, lakini Tanzania siyo na ndiyo maana kila wikiendi timu moja kubwa inafungwa na timu zinazochukuliwa kama ndogo,” amesema.
  Amesifu ushindani huo kwamba ni mzuri na unamsaidia mchezaji kuwa bora kila wakati ili kuhimili ushindani.  Imbem kwa sasa anacheza michuano ya kila mwaka ya Koth Biro nchini Kenya kutokana na Ligi ya Tanzania kusimama.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LIGI YA TANZANIA BORA KULIKO YA KENYA, ASEMA IMBEM WA COASTAL ALIYETOKEA KPL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top