• HABARI MPYA

  Tuesday, December 02, 2014

  HANS POPPE: NATAMANI MTANI JEMBE IWE KESHO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema anatamani mechi ya Nani Mtani Jembe 2 dhidi ya mahasimu wao, Yanga SC iwe hata kesho.
  Kauli hiyo ya Hans Poppe inakuja baada ya Simba SC kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Daniel Muzeyi ‘Dan’ Sserunkuma kwa Mkataba wa miaka miwili.
  “Natamani mechi ya Nani Mtani Jembe iwe hata kesho,”amesema Hans Poppe huku akichekelea kwa furaha kuashiria wino wa Sserunkuma unampa ‘qibli’ kuelekea mechi hiyo wiki ijayo.
  Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) alikuwa Ulaya kwa mapumziko na baada ya kurejea juzi, Simba SC inaanika usajili wa kwanza wa mchezaji mpya.
  Hans Poppe kushoto akiwa na Rais wa Simba SC, Evans Aveva na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Said Tuliy na Collins Frisch
  Dan Sserunkuma akifanyiwa vipimo vya afya kabla ya kusaini Simba SC


  Mzaliwa huyo wa Desemba 4, mwaka 1989 mjini Kampala, Uganda amesaini Mkataba huo baada ya kumaliza Mkataba na klabu ya Gor Mahia ya Kenya.
  Sserunkuma ni mchezaji aliyezaliwa na kukulia wilaya ya Lubega mjini Kampala na alisoma shule maarufu iliyoibua vipaji vya nyota wengi Uganda, St. Mary's ya Kitende.
  Nyota kibao wanaotamba kisoka Uganda wamepita shule hiyo kama Joseph Owino, David Obua, Eric Obua, Emmanuel Okwi na Ibrahim Juma.
  Pia utotoni mwake, alipitia katika akademi ya Friends of Football akiwa ana umri wa miaka 10, kabla ya kuchezea Express kuanzia 2008 hadi 2011 alipohamia Victors alikocheza hadi 2012 alipokwenda Kenya kujiunga na Nairobi City Stars hadi mwaka 2012 alipotua Gor Mahia.
  Sserunkuma ni mfungaji bora mara mbili mfululizo kwa misimu miwili iliyopita ya Ligi Kuu ya Kenya, wakati pia mwaka 2012 alikuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya nchi hiyo.
  Mwaka 2013, Sserunkuma alishinda tuzo ya Mchezaji Bora Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (USPA) Uganda, akiwapiku Tony Mawejje aliyekuwa anacheza Norway na mshambuliaji wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbarara (MUST), Siraje Muhindo.
  Sserunkuma anachukua nafasi ya majeruhi Mkenya, Paul Kiongera ambaye Simba SC imeamua kumuondoa katika usajili hadi hapo atakapopona goti kuanzia Machi mwakani, ili arejeshwe kwa ajili ya msimu ujao.
  Wachezaji wengine wa kigeni Simba SC ni Waganda Joseph Owino, Emmanuel Okwi na Warundi Pierre Kwizera na Amisi Tambwe- ambao pamoja na Sserunkuma wanakamilisha idadi ya kikanuni ya Ligi Kuu ya wachezaji watano wa nje.
  Lakini tayari kiungo mshambuliaji wa Gambia, Omar Mboob yuko kwenye majaribio Simba SC tangu jana na kama akifuzu anaweza kuchukua nafasi ya Kiongera, ambaye hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HANS POPPE: NATAMANI MTANI JEMBE IWE KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top