• HABARI MPYA

    Sunday, November 16, 2014

    NOOIJ KUVUNA NINI LEO SOMHLOLO MECHI YA 10 TAIFA STARS?

    Na Mwandishi Wetu, MBABANE
    KOCHA Mholanzi, Mart Nooij leo anatarajiwa kuiongoza timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika mchezo wa 10 tangu aanze kazi Aprili mwaka huu, akirithi mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen.
    Stars itakuwa mgeni wa Swaziland kwenye Uwanja wa Taifa wa Somhlolo mjini Mbabane katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa ulio katika kalenda ya FIFA.
    Kikosi cha wachezaji 23 wa Taifa Stars kilipitia mjini Johannesburg, Afrika Kusini kwa kambi fupi kabla ya kutua Mbabane Ijumaa ambako baada ya mechi leo, kesho kitarejea nyumbani.
    Taifa Stars wakiwa mazoezini mjini Mbabane jana tayari kwa mechi leo

    Kikosi hicho kinaundwa na makipa Aishi Manula (Azam) na Deogratias Munishi (Yanga). Mabeki ni Abubakar Mtiro (Kagera Sugar), Aggrey Morris (Azam), Emmanuel Simwanda (African Lyon), Hassan Isihaka (Simba), Kevin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Osacr Joshua (Yanga), Said Mourad (Azam), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Shomari Kapombe (Azam).
    Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Haruna Chanongo (Simba), Himid Mao (Azam), Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar), Said Ndemla (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
    Washambuliaji ni Juma Luizio (ZESCO, Zambia), Mbwana Samata (TP Mazembe, DR Congo), Simon Msuva (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).
    Mart Nooij ataiongoza Taifa Stars kwa mara ya 10 leo ikimenyana na Swaziland mjini Mbabane

    Tayari Nooij amekwishaiongoza Stars katika mechi tisa, kati ya hizo akishinda tatu, sare tatu na kufungwa tatu.
    Nooij alianza kwa sare ya 0-0 na Malawi katika mchezo wa kirafiki mjini Mbeya, kabla ya kushinda 
    1-0 dhidi ya Zimbabwe mchezo wa kufuzu AFCON mjini Dar es Salaam.
    Akashinda tena 1-0 na Malawi katika mchezo wa kirafiki Dar es Salaam kabla ya sare ya 2-2 na Zimbabwe kufuzu AFCON mjini Harare na baadaye kufungwa 4-2 na Botswana katika mchezo wa kirafiki mjini Gaborone.
    Akatoa sare ya 2-2 na Msumbiji mjini Dar es Salaam kufuzu kabla ya kwenda kufungwa 2-1 katika mchezo wa marudiano mjini Maputo na kisha kufungwa 2-0 na Burundi mchezo wa kirafiki mjini Bujumbura.
    Mechi iliyopita, Nooij aliiongoza Stars kushinda kwa kishindo, mabao 4-1 dhidi ya Benin, ukiwa pia mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Tutarajie nini katika mchezo wa 10 wa Mholanzi huyo leo Mbabane? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NOOIJ KUVUNA NINI LEO SOMHLOLO MECHI YA 10 TAIFA STARS? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top