• HABARI MPYA

    Sunday, November 16, 2014

    AZAM FC NA YANGA SC WANAKITUMIAJE KIPINDI HIKI?

    TANZANIA mwaka huu imeendeleza utamaduni wake wa kufanya vibaya kwenye michuano ya Afrika, baada ya wawakilishi wake wote, Yanga SC na Azam FC kutolewa mapema.
    Azam FC iliyocheza Kombe la Shirikisho, ilitolewa na Ferroviario de Nampula katika hatua ya awali kwa kufungwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 1-0 nyumbani kabla ya kwenda kufungwa 2-0 ugenini.
    Yanga SC angalau walifika hatua ya pili, 32 Bora ambako walitolewa na Al Ahly ya Misri kwa penalti baada ya sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
    Ukweli ni kwamba mwaka huu, Yanga SC walijitahidi tofauti na utamaduni wao wa kunyanyaswa na timu za Kaskazini mwa Afrika miaka nenda, rudi.

    Angalau kwa mara ya kwanza mwaka huu Yanga SC iliweka rekodi ya kupata ushindi wa kwanza mbele ya timu ya Kaskazini 1-0, Dar es Salaam.
    Lakini kwa sababu ilitolewa, ukweli unabaki pale pale kwamba Tanzania imeendeleza utamaduni wake wa kuboronga kwenye michuano ya Afrika.
    Bahati yao Yanga SC na Azam wataiwakilisha tena nchi mwakani kwenye michuano ya Afrika, wakibadilishana tu njia. Azam watacheza Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza mwakani, wakati Yanga SC watahamia kwenye Kombe la Shirikisho.
    Mara ya mwisho Tanzania kucheza hatua ya makundi ya michuano ya Afrika ilikuwa mwaka 2003 wakati Simba SC ilipofika hatua hiyo.
    Na hiyo ilikuwa mara ya pili kihistoria kwa klabu za Tanzania, baada ya Yanga SC kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kufika hatua hiyo mwaka 1998, wote Ligi ya Mabingwa.
    Zaidi ya hapo, wakati wa mfumo wa zamani wa michuano ya Afrika, Yanga SC walifika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara mbili 1969 na 1970, wakati Simba SC ilifika Nusu Fainali mwaka 1974.
    Yanga SC ilifika pia Robo Fainali ya iliyokuwa michuano ya Kombe la Washindi mwaka 1996 na Simba SC ilifika fainali ya iliyokuwa michuano ya Kombe la CAF.
    Simba SC inabaki kuwa klabu ya kihistoria Tanzania kwa mafanikio yake kwenye michuano ya Afrika- kwa kuweza kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika na Fainali ya Kombe la CAF.
    Nchi nyingine barani zina nafasi zaidi ya moja za kuingiza timu kwenye michuano ya Afrika kutokana na kufanya kwao vizuri kwenye michuano hiyo, lakini Tanzania inaingiza timu moja kwenye kila michuano, kwa sababu haina makali.
    Ili kuweza kuongezewa nafasi za kushiriki michuano hiyo, lazima tupate matokeo mazuri na timu zetu zicheze hatua ya makundi.
    Lakini hilo limekuwa gumu miaka nenda, rudi kwa sababu bado klabu zetu hazijaonyesha dhamira haswa ya kuingia kwa ajili ya kushindana kwenye michuano hiyo.
    Yanga SC mwaka huu walidhamiria kubadilisha utamaduni wa kunyanyaswa na timu za Kaskazini, wakawa na maandalizi mazuri na wakafanikiwa kwa kuanzia kushinda mechi ya kwanza dhidi ya timu hizo.
    Na walikaribia kabisa kuitoa Ahly, kama si Said Bahanuzi na Oscar Joshua kupoteza penalti zao.
    Matunda ya dhamira wameyavuna Yanga SC mwaka huu, lakini vyema huo ukawa mwanzo tu, kwa kuweka dhamira ya kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano ya Afrika.
    Azam FC mwaka jana walifika hatua ya 16 Bora, lakini mwaka huu wametolewa hatua ya awali tu, nadhani mafanikio ya awali yaliwalevya.
    Lakini si kitu, wahenga wanasema watu wanajifunza kutokana na makosa, bila shaka timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake mwakani itazinduka.
    Kwa sasa, Ligi Kuu ya Bara imesimama tangu wiki iliyopita na itarejea tena mwishoni mwa Desemba, wakati michuano ya Afrika itaanza mapema mwakani.
    Wachezaji wa timu zote za Ligi Kuu wamepewa mapumziko ya mafupi na wanatarajiwa kuanza kurejea kwenye klabu zao mwishoni mwa wiki. 
    Dirisha dogo la usajili wa nyumbani nalo limefunguliwa jana- maana yake hiki ni kipindi kizuri kwa wawakilishi wetu hao wa michuano ya Afrika kujitathmini baada ya mechi saba za awali za Ligi Kuu.
    Baada ya kujitathmini, Yanga na Azam FC wafanye maandalizi ya kuifikiria michuano ya Afrika na si fikra kubakia kwenye Ligi Kuu ya Bara pekee.
    Kama ni kusajili wachezaji, basi wasajiliwe aina ya wachezaji ambao watamudu kucheza michuano hiyo ya Afrika na kuzisaidia timu hizo kufanya vizuri.
    Ukweli ni kwamba kutokuwa na klabu imara nchini kwa kiasi kikubwa kunachangia hata kuzorota kwa tmu yetu ya taifa- kwa sababu ni wachezaji hao hao wa klabu ndio wanatakiwa wachezee timu za taifa.
    Hivyo basi, kama kuna kipindi kizuri cha maandalizi kuelekea michuano ya Afrika kwa wawakilishi wetu, Azam FC na Yanga SC, basi ni hiki. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC NA YANGA SC WANAKITUMIAJE KIPINDI HIKI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top