• HABARI MPYA

    Wednesday, November 26, 2014

    AFCON HATUMO, HATA CHALLENGE HATUCHEZI?

    NOVEMBA inayoyoma hii, hakuna taarifa yoyote mpya kuhusu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge.
    Mara ya mwisho, Katibu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye aliibuka na kusema anazungumza na Sudan, wataipokea uenyeji Ethiopia iliyojitoa.
    Tangu wakati huo, Musonye siyo tu hajaibuka tena, hata simu yake akipigiwa na Waandishi wa Habari hapokei. Labda Wakenya wenzake.

    Tunasikia tu mipango ya chinichini inaendelea, Tanzania inashawishiwa ipokee uenyeji wa michuano hiyo. Na tunasikia pia minong’ono Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesema dira yake ni mashindano ya CAF- maana yake CECAFA wameula wa chuya.
    Ethiopia iliomba na kupewa uenyejji wa michuano hiyo mwaka jana, lakini ghafla miezi miwili kabla ya kupokea ugeni wakajitoa. Kwa tatizo lipi, ni siri yao wao na CECAFA.
    Najiuliza, ukanda wetu huu una laana ya nani hata kila jambo haliendi vizuri?  
    Tunashindwa kufanya Challenge yetu, wakati tayari kwa mara nyingine tena, hatutakuwa na mwakilishi kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, kufuatia timu zetu zote kutolewa mapema.
    Tanzania na Kenya hazikufanikiwa hata kufika hatua ya makundi kuwania fainali hizo, wakati Uganda angalau walipigana hadi siku ya mwisho ya kufuzu.
    The Cranes walishindwa kutimiza ndoto za kucheza tena Fainali za Mataifa ya Afrika tangu ilipocheza mara ya mwisho mwaka 1978, kufuatia kuzidiwa kete na Guinea.
    Ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja, baada ya Nahodha Andy Mwesigwa kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kucheza rafu, Uganda ilichapwa mabao 2-0 na wenyeji Guinea katika mchezo wa Kundi E kufuzu AFCON.
    Mabao ya Guinea yalifungwa na Ibrahima Traore dakika ya 29 na Seydouba Soumah dakika ya 61 kwa penalti baada ya rafu ya Mwesigwa kwenye boksi dakika ya 59.
    Guinea iliyomaliza na pointi 10, imeungana na Ghana iliyoongoza Kundi kwa pointi zake 11 kwenda Equatorial Guinea kwenye fainali za AFCON mapema mwakani.
    Kwa ujumla, katika nchi 11 wanachama wa CECAFA, Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia, Rwanda, Burundi, Eritrea, Sudan Kusini, Djibouti na Somalia hakuna hata moja iliyofuzu. Zanzibar si mwanachama wa FIFA, haichezi mechi za kimataifa, kwa kuwa inachukuliwa kama sehemu ya Tanzania.
    Huu ni mwendelezo wa kudidimia kwa soka ya ukanda wa CECAFA, ambayo mwanzoni mwa historia ya michuano hiyo ilikuwa juu.
    Angalau, katika wanachama wa CECAFA, ni Sudan na Ethiopia ambazo zimeendelea kidogo kututoa kimasomaso kwenye michuano ya kimataifa.
    Sudan wanafanya vizuri hadi kwenye michuano ya klabu, ambako wana nafasi zaidi ya moja kuingiza klabu kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.  
    Uganda wamecheza AFCON tano, 1962 waliposhika nafasi ya nne, 1968,
    1974, 1976 walipokomea Raundi ya Kwanza na hiyo ya kufika fainali 1978.
    Kenya pia wamecheza mara tano, 1972, 1988, 1990, 1992 na 2004 mara zote wakikomea Raundi ya Kwanza, wakati Tanzania imecheza mara moja tu 1980 sawa na Rwanda 2004.
    Sudan wamecheza mara nane fainali hizo, 1957 walipokuwa washindi wa tatu, 1959 washindi wa pili sawa na 1963, 1970 walipochukua ubingwa,
    1972 walipokomea Raundi ya Kwanza sawa na 1976 na 2008 wakati mara ya mwisho walipokwenda AFCON 2012 walifika Robo Fainali.
    Ethiopia walikuwepo kwenye fainali za mwaka jana wakatolewa Raundi ya Kwanza na walicheza pia AFCON za 
    1957 wakawa washindi wa pili, 1959 wakawa wa tatu, 1962 walipokuwa mabingwa, 1963 walipokuwa wa nne, 1965 walikomea Raundi ya Kwanza, 1968 walipokuwa wa nne, 1970 walipokomea Raundi ya Kwanza sawa na 1976,  1982 na 2013.
    Angalau Sudan na Ethiopia zina pa kuhemea, lakini hali mbaya kwa Tanzania, Kenya, Uganda na wanachama wengine wa CECAFA.
    Miaka ya nyuma kabla ya mfumuko wa makampuni ya kibiashara na wawekezaji wengi kuja barani, ulikuwa unaweza kuelewa mashindano yakikwama kwa sababu ya fedha, lakini katika dunia ya leo kushindwa kufanya Challenge ni fedheha.
    Maana yake, viongozi wa CECAFA hawajishughulishi na masuala ya bodi hiyo kikamilifu na pengine Nairobi si mahala salama sana kuwa makao makuu ya Baraza.
    Ndugu zetu Wakenya wanahodhi kila kitu katika Sekretarieti kwa miaka sasa, lakini mambo hayaendi sawa CECAFA na bila shaka huu ni wakati mwafaka sasa ofisi zihame huko na sura za watendaji zibadilike.
    CECAFA haihitaji watu kwa ajili ya kupanga ratiba tu na kugawa ‘free pass’, inahitaji watendaji wa shughuli za kila siku za bodi kwa manufaa ya soka ya ukanda huu. Angalia sasa, AFCON hatumo, hata Challenge hatuchezi, balaa gani hili! 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AFCON HATUMO, HATA CHALLENGE HATUCHEZI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top