• HABARI MPYA

  Sunday, November 23, 2014

  MCHEZAJI WANAYEMTAKA AZAM ANALIPWA MILIONI 300 KWA MWAKA, MSHAHARA MILIONI 16 KWA MWEZI EL MERREIKH

  Na Samira Said, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Azam huenda wakahitajika kuvunja benki yao endapo wanataka kumsajili mshambuliaji wa timu ya El Merreikh ya Sudan, Mohammed Traore, imefahamika.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY kwa simu kutoka Khartoum, Sudan leo, Ofisa Habari wa El Merreikh, Babiker Osman, amesema kuwa mshambuliaji huyo ana mkataba wa miaka mitatu na mabingwa hao wapya wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) utakaomalizika Desemba 2016.
  Osman  amesema kuwa Traore alisaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea klabu hiyo kwa kulipwa kila mwaka Dola za Marekani 180,000 (Sh. Milioni 300)na mshahara wa mwezi Dola za Marekani 10,000 (Sh. Milioni 16).
  " Traore ni mchezaji mzuri na mchezaji mkubwa, tumepokea barua ya Azam lakini viongozi wa juu hawajaizungumzi kwa sababu ni mshambuliaji wanayemhitaji sana kipindi hiki", alisema Osman.
  Azam FC inamtaka Mohamed Traore (kulia) anayeliwa Sh. Milioni 300 kwa mwaka Merreikh mbali na mshahara wa Sh. Milioni 16,000 kwa mwezi

  Aliongeza kuwa Traore kwa sasa anaonekana anatazama zaidi maslahi na si ukubwa wa nchi au jina la klabu.
  " Si Azam peke yake ambao wanamtaka Traore, wengi wamevutiwa na ubora wake akiwa na timu yake ya Taifa ya Mali, ila anaangalia sana ofa na si jambo lingine," aliongeza msemaji huyo.
  Alimtaja Traore kuwa ndiye mchezaji anayeongoza katika orodha ya wafungaji kwenye Ligi Kuu ya Sudan akiwa amefunga mabao 15.
  Mshambuliaji huyo mwenye miaka 20 aliisaidia El Merreikh kutwaa ubingwa wa Super Cup katika mechi iliyofanyika mapema mwezi huu na kushinda kikombe cha nne mfululizo.
  Hata hivyo wapinzani wa El Merreikh, timu ya El Hilal ndio wanaongoza ligi kwa sasa.
  Tayari Azam imefanikiwa kumnasa beki wa El Merreikh, Pascal Serge Wawa, ambaye alisaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea timu hiyo ya Chamazi jijini Dar es Salaam.
  Azam inajipanga kuimarisha kikosi ili iweze kutetea ubingwa wake wa Bara na kufanya vizuri katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika watakayoshiriki mapema mwakani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MCHEZAJI WANAYEMTAKA AZAM ANALIPWA MILIONI 300 KWA MWAKA, MSHAHARA MILIONI 16 KWA MWEZI EL MERREIKH Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top