• HABARI MPYA

  Thursday, November 20, 2014

  YANGA SC 'TUMBO JOTO' KWA SIMBA NANI MTANI JEMBE 2

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAKATI kampeini ya ‘Na Mtani Jembe2’, ikiendelea kushika kasi kwa timu kongwe Simba na Yanga, mashabiki wa klabu ya Yanga wameitaka Kamati ya Usajili kufanya usajili mzuri kama wanahitaji kumfunga Simba katika mchezo huo.
  Simba na Yanga zinatarajiwa kushuka dimbani Disemba 13 katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuwania taji hilo la Nani Mtani Jembe linaloratibiwa na wadhamini wakuu wa timu hizo bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambayo inawapa mashabiki nafasi ya kuziona timu hizo mara tatu kwa mwaka.

  Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Jijini Dar es Salaam jana, Mwanachama wa Yanga Wazir Jittu ambaye ni Katibu wa Tawi la Tandale, alisema kuwa, wao hawana shaka na kampeini hiyo ambayo inawapa fursa ya kukutana na watani wao Simba, ila wasiwasi wake ni juu ya Kamati yake ya usajili kwani imekaa kimywa wakati inatambua wana mchezo mgumu.
  Jittu alisema, mpaka sasa anaziona dalili za kufungwa na Simba, kutokana na usajili ambao wameufanya na kuendelea kuufanya, na kusema kuwa, atapata amani baada ya kamati ya Yanga ya usajili itakapoanza kufanya usajili, kwani hata msimu uliopita walisajili nyota wawili pekee ambao hawana faida ndani ya timu yao.
  “Mimi kwanza nawapongeza mno Kilimanjaro kwa kuandaa kitu kizuri kama hiki, sisi kwetu ni fursa ya kipekee kupata mechi ya tatu ya watani, na pia kutukutanisha, ila nawaomba viongozi Yanga wanafye usajili bila hivyo Simba atatufunga tena,”alisema.
  Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Simba Tawi la Wekundu wa Terminal ‘Mwanzo Mwisho’ Justine Joel, anakiri Simba itawafunga Yanga kwani licha ya kuzidiwa katika kubutana wao, wameelekeza nguvu zao uwanjani kwani wanahitaji mataji yazidi kuwepo makao makuu ya klabu yao.
  “Yanga kumfunga Simba, ni ndoto jamani, mie nakwambia, Simba ilikuwa mbovu kipindi flani lakini tulitoka sare ya mabao 3-3 na Yanga iliyokuwa inajiita nzuri, wao wakae wasubiri kichapo tu, Simba tuko vizuri mno,”alisema Joel.
  Huku Bakiri Bakere Mwenyekiti wa Vijana wa Yanga, alisema kuwa, uwepo wa kocha wao Marcio Maximo na wachezaji wao wa Kibrazil Gelson Santos ‘Jaja’ na mwenzake Andrey Coutinho ni moja ya ushindi, na kusema kuwa Simba hawana kikosi cha kuwatisha katika mchezo huo kwani wao wako kamili kuwavaa.
  Naye Ustadh Masoud Mwenyekiti wa Tawi la Mpira Pesa, alisema kuwa, wao walishaanza matokeo siku nyingi hasa kwa kutambua mchezo wanaokuja kuucheza ni wa kiushindani zaidi, na wanahitaji kuwafunga zaidi ya mabao 3-1 waliyowafunga msimu uliopita na hilo linawezekana kwani wanaimani kubwa na kikosi chao.
  Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager alisema mashabiki wanatakiwa kuzipigia kura timu zao ili ziweze kushinda kitita cha shilingi milioni 80 ambazo pia watakabidhiwa pamoja na kombe. "Kupigia kura timu yako unatakiwa kufungua bia ya Kilimanjaro Premium Lager na kuandika neno Simba au Yanga ikifuatiwa na namba iliyoko chini ya kizibo kwenda namba 15415. Kwa kufanya hivyo takuwa umepunguza kiasi cha shilingi 10,000 kutoka timu pinzani na kuiongezea timu uipendayo".  
  “Msimu huu ni wa kipekee sana maana tumeona bora atakayefungwa siku ya mechi ya Nani Mtani Jembe walau apate kifuta jasho cha sh mil 5 huku mshindi akipata milioni 15. Klabu itanufaika, wachezaji watanufaika na mashabiki watanufaika. Sasa ni kazi kwenu viongozi kuwahamasisha mashabiki wa timu zenu,”alisema Kavishe.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC 'TUMBO JOTO' KWA SIMBA NANI MTANI JEMBE 2 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top