• HABARI MPYA

  Sunday, November 30, 2014

  USHAURI WA BURE KWA TENGA NA CECAFA YAKE

  OFISA Habari wa Katibu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Rodgers Mulindwa ameibuka wiki hii kukanusha taarifa za magazeti ya kwao, Uganda kuhusu Kombe la Challenge.
  Mulindwa anadai kuna mwandishi amemlisha maneno na kuandika kwamba amesema Challenge haitafanyika- na anakanusha.
  Mara kadhaa Mulindwa amekuwa na matatizo na Waandishi wa Habari, si wa kwao tu, hata wa nchi nyingine- kwa hiyo tunamuachia hayo kama matatizo yake. 
  Na pamoja na kujibizana na magazeti ya kwao, Mulindwa akasema CECAFA chini ya Mwenyekiti wake, Leodegar Tenga na Katibu, Nocholas Musonye bado inahangaikia kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika mwaka huu.

  Leo ni Novemba 30, kwa kawaida ya kalenda ya Challenge, wakati kama huu huwa tayari mashindano yanakuwa yameanza.
  Achana na hizi ‘longologo’ za Mulindwa, mara ya mwisho, mapema Novemba Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye aliibuka na kusema anazungumza na Sudan, wataipokea uenyeji Ethiopia iliyojitoa.
  Tangu wakati huo, Musonye siyo tu hajaibuka tena, hata simu yake akipigiwa na Waandishi wa Habari hapokei. Labda Wakenya wenzake.
  Tunasikia tu mipango ya chinichini inaendelea, Tanzania inashawishiwa ipokee uenyeji wa michuano hiyo. Na tunasikia pia minong’ono Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesema dira yake ni mashindano ya CAF- maana yake CECAFA wameula wa chuya.
  Ethiopia iliomba na kupewa uenyejji wa michuano hiyo mwaka jana, lakini ghafla miezi miwili kabla ya kupokea ugeni wakajitoa. Kwa tatizo lipi, ni siri yao wao na CECAFA.
  Tunashindwa kufanya Challenge yetu, wakati tayari kwa mara nyingine tena, hatutakuwa na mwakilishi kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, kufuatia timu zetu zote kutolewa mapema.
  Tanzania na Kenya hazikufanikiwa hata kufika hatua ya makundi kuwania fainali hizo, wakati Uganda angalau walipigana hadi siku ya mwisho ya kufuzu.
  The Cranes walishindwa kutimiza ndoto za kucheza tena Fainali za Mataifa ya Afrika tangu ilipocheza mara ya mwisho mwaka 1978, kufuatia kuzidiwa kete na Guinea.
  Ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja, baada ya Nahodha Andy Mwesigwa kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kucheza rafu, Uganda ilichapwa mabao 2-0 na wenyeji Guinea katika mchezo wa Kundi E kufuzu AFCON.
  Mabao ya Guinea yalifungwa na Ibrahima Traore dakika ya 29 na Seydouba Soumah dakika ya 61 kwa penalti baada ya rafu ya Mwesigwa kwenye boksi dakika ya 59.
  Guinea iliyomaliza na pointi 10, imeungana na Ghana iliyoongoza Kundi kwa pointi zake 11 kwenda Equatorial Guinea kwenye fainali za AFCON mapema mwakani.
  Kwa ujumla, katika nchi 11 wanachama wa CECAFA, Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia, Rwanda, Burundi, Eritrea, Sudan Kusini, Djibouti na Somalia hakuna hata moja iliyofuzu. Zanzibar si mwanachama wa FIFA, haichezi mechi za kimataifa, kwa kuwa inachukuliwa kama sehemu ya Tanzania.
  Huu ni mwendelezo wa kudidimia kwa soka ya ukanda wa CECAFA, ambayo mwanzoni mwa historia ya michuano hiyo ilikuwa juu.
  Angalau, katika wanachama wa CECAFA, ni Sudan na Ethiopia ambazo zimeendelea kidogo kututoa kimasomaso kwenye michuano ya kimataifa.
  Sudan wanafanya vizuri hadi kwenye michuano ya klabu, ambako wana nafasi zaidi ya moja kuingiza klabu kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.  
  Uganda wamecheza AFCON tano, 1962 waliposhika nafasi ya nne, 1968,
  1974, 1976 walipokomea Raundi ya Kwanza na hiyo ya kufika fainali 1978.
  Kenya pia wamecheza mara tano, 1972, 1988, 1990, 1992 na 2004 mara zote wakikomea Raundi ya Kwanza, wakati Tanzania imecheza mara moja tu 1980 sawa na Rwanda 2004.
  Sudan wamecheza mara nane fainali hizo, 1957 walipokuwa washindi wa tatu, 1959 washindi wa pili sawa na 1963, 1970 walipochukua ubingwa,
  1972 walipokomea Raundi ya Kwanza sawa na 1976 na 2008 wakati mara ya mwisho walipokwenda AFCON 2012 walifika Robo Fainali.
  Ethiopia walikuwepo kwenye fainali za mwaka jana wakatolewa Raundi ya Kwanza na walicheza pia AFCON za 
  1957 wakawa washindi wa pili, 1959 wakawa wa tatu, 1962 walipokuwa mabingwa, 1963 walipokuwa wa nne, 1965 walikomea Raundi ya Kwanza, 1968 walipokuwa wa nne, 1970 walipokomea Raundi ya Kwanza sawa na 1976,  1982 na 2013.
  Angalau Sudan na Ethiopia zina pa kuhemea, lakini hali mbaya kwa Tanzania, Kenya, Uganda na wanachama wengine wa CECAFA.
  Inavyoonekana, kwa sasa CECAFA imeshindwa kuubeba mzigo wa Challenge na pia inaelemewa na michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
  Hapo hapo tukumbuke kwamba, CECAFA wanatakiwa kuendesha mashindano ya vijana na wanawake, lakini wameshindwa kwa sababu zile zile ambazo zinaelekea kuwafanya washindwe kufanya Challenge na Kagame.
  Leo nataka nawapa ushauri bure CECAFA, ili japo tuokoe Challenge na Kagame. Wabadilishe mfumo wa uendeshaji wa mashindano hayo, kuliko kuipa nchi mzigo wa uenyeji wa michuano yote, waweke utaratibu nafuu na wa kisasa zaidi.
  Challenge ichezwe kwa mfumo wa nyumbani na ugenini kwa mtoano hadi kubaki timu mbili za kuingia fainali.
  Tugawe makundi mawili, nchi zicheze mechi nyumbani na ugenini, vinara wa makundi, wakutane katika fainali ambayo itafanyika katika mji ulioteuliwa na CECAFA kuwa mwenyeji wa mechi moja tu ya fainali.
  Ni wajibu wa CECAFA sasa kupitia kalenda za CAF na FIFA na kutafuta namna ya kuweka ratiba ya Challenge vizuri bila kugongana na mashindano mengine.
  Vile vile kwa Kombe la Kagame, klabu zicheze nyumbani na ugenini katika makundi mawili, baadaye timu mbili za juu ziende Nusu Fainali, ambayo pia itachezwa nyumbani na ugenini na baadaye Fainali, ambayo pia kila timu itacheza mechi moja nyumbani.
  Hapa pia ni wajibu wa CECAFA, kupitia kalenda za mashindano mengine ya CAF na FIFA, ili kuhakikisha ratiba ya Kombe la Kagame haiingiiliani na michuano mingine. Kwa timu kucheza nyumbani itawasaidia kupata mapato ya milangoni, na katika kila mechi kutakuwa na fungu la fedha linalokwenda CECAFA, ambalo mwisho wa siku litasaidia kuandalia fainali.
  Na bila shaka mashindano yatapata msisimko zaidi na kuvutia tena wadhamini, kwa sababu sifikirii makampuni ya kuuza pombe yatakuwa tayari kuweka fedha zao mashindano yakifanyika katika nchi ambazo ‘Pombe ni haramu’ kama Sudan na Zanzibar.   
  Huo ni ushauri wangu mimi Mtanzania mmoja, Mahmoud Ramadhani Zubeiry, mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam. Na ni ushauri wa bure kabisa kwa CECAFA. Uwafikie, wafikishiwe.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: USHAURI WA BURE KWA TENGA NA CECAFA YAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top