• HABARI MPYA

  Monday, November 24, 2014

  TUZO ZA FILAMU TANZANIA ZAZINDULIWA RASMI

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  TUZO za filamu Tanzania zimezinduliwa rasmi mjini Dara es Salaam jana kwa shamra shamra za aina yake, zilizohudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel
  Uzinduzi huo uliohudhuriwa na wadau, wasanii na wageni mbalimbali wanaounga mkono tasnia hiyo hapa nchini, ni ishara  rasmi kuwa pazia la tuzo hizo zinazotarajiwa kufanyika mwakani sasa liko wazi.
  Tuzo hizo ambazo hazijawahi kutokea nchini zimeandaliwa na Shirikisho la Filamu Tanzania kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania chini ya usimamizi wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo. 
  Wasanii Yussuf Mlela, Monalisa na Flora walihudhuria pia jana 

  Naibu katibu mkuu wa Wizara ya Habari, vijana, utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel, akiongea neno wakati wa uzinduzi

  Tuzo hizo zitakazoshindaniwa katika vipengele zaidi ya Thelathini (30), hii ni nafasi nzuri na yakipekee kwa wana tasnia ya filamu nchini na kuonesha ukomavu na kukubalika kwa tasnia hiyo nchini. Tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika mapema 2015 jijini Dar es Salaam na zitakuwa zikifanyika kila mwaka.
  Akiongea katika uzinduzi huo kwa niaba ya Waziri wa Habari, vijana, utamaduni na michezo, Naibu katibu mkuu wa wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa tasnia ya filamu imepiga hatua kubwa nchini na hata nje ya nchi kwani kazi inaonekana. “Kwanza kabisa niwapongeze Shirikisho la Filamu Tanzania kwa kuandaa tuzo hizi zitakazoleta ufanisi katika tasnia ya filamu nchini. Nina Imani kuwa mmejipanga kukabiliana na changamoto katika soko la kimataifa, hii ni kuwa tayari na kujiandaa kukamilifu kukabiana nazo kwa kuwa na kazi zenye ubora mkubwa, kutambulika kimataifa kwa uzuri wa kazi mnazozifanya, kutangaza nchi yetu kimataifa kupitia filamu na hata kuongeza pato la taifa kwa kazi zenu.”
  Naye Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifwamba alisema kuwa wanayofuraha kubwa kama shirikisho kuandaa tuzo hizo kwani inaonesha kukua kwa soko la filamu nchini kwa kasi na hata kuleta tija katika jamii. “Tunawashukuru wote mliofika kutuunga mkono katika ufunguzi rasmi wa tuzo hizi za Filamu nchini, kwa namna ya pekee tunawashukuru wadhamini wetu Sadolin Paints, Appex, na Hak neel, tunaomba wadau wengi zaidi wajitokeze kudhamini tuzo hizi kwani ni kuonesha uzalendo kwa kupenda na kuthamini vya nyumbani. Kwa kufanya hivyo tutakua tumeunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na wadau wa tasnia hii ya filamu nchini,” alisema Mwakifwamba.
  Hii ni fursa pekee kwa wadau wa Tasnia ya filamu nchini kukuza na kutangaza kazi zao katika soko la kimataifa hivyo hawana budi kuichangamkia fursa hii kwa kupeleka kazi zao walizozifanya na kujaza fomu ili kuingia katika kinyang’anyiro cha tuzo hizo kubwa nchini katika tasnia hiyo. Fomu zinapatikana katika ofisi za Shirikisho la Filamu Tanzania zilizopo mtaa wa Ikungi-Kinondoni B jijini Dar es Salaam au waweza pata katika mtandao kwa kutembelea www.taff.or.tz. Mwisho wa kujiandikisha ushiriki na kuwasilisha kazi katika kuwania tuzo hizo ni 15/12/2014.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TUZO ZA FILAMU TANZANIA ZAZINDULIWA RASMI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top