• HABARI MPYA

  Tuesday, November 25, 2014

  KIUNGO YANGA SC ATIMKIA MALAYSIA LEO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa zamani wa Yanga SC, Abdi Kassim Sadallah ‘Babbi’ ameondoka jioni ya leo kwenda kufanya mipango ya kujiunga na klabu ya Sabah ya Ligi Kuu ya Malaysia.
  Babbi ambaye amemaliza Mkataba na Uitm FC aliyoichezea msimu uliopita, iwapo atafikia makubaliano katika mazungumzo, atafanyiwa vipimo vya afya ambavyo akifuzu pia atapewa Mkataba.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jioni ya leo Dar es Salaam wakati anaondoka, mchezaji huyo wa kimataifa wa Tanzania, alisema kwamba Sabah ilivutiwa naye baada ya kumuona wakati anachezea Uitm.
  Abdi Kassim 'Babbi' ameondoka leo kwenda Malaysia kutafuta kazi

  “Jamaa waliniona wakati nacheza kule, wakawa wananitaka muda mrefu, isipokuwa Mkataba ulikuwa unanibana, ila baada ya kumaliza Mkataba wangu kule, sasa nakwenda kuwasikiliza,”amesema Babbi.
  Babbi ambaye pia anafahamika kama Ballack wa Unguja, akifananishwa na kiungo wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani, Michael Ballack ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao katika Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kufunguliwa mwaka 2007.
  Babbi alifunga bao hilo Septemba 1, mwaka 2007 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Uganda, The Cranes- enzi hizo Taifa Stars ikifundishwa na kocha Mbrazil, Marcio Maximo ambaye kwa sasa yupo Yanga SC.
  Babbi aliibukia Mlandege ya Zanzibar mwaka 2002 kabla ya 2004 kuhamia Mtibwa Sugar ya Morogoro ambako alidumu hadi 2007 aliponunuliwa na vigogo wa Tanzania, Yanga SC.
  Mwaka 2011 Babbi aliuzwa Dong Tam Long Anya Vietnam ambako alicheza hadi 2012 aliporejea nyumbani kujiunga na Azam FC.
  Mwaka 2013, Babbi alikwenda KMKM kabla ya mapema mwaka huu kujiunga na UiTM FC ambayo baada ya kumaliza Mkataba wake wa mwaka mmoja ameamua kuachana nayo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIUNGO YANGA SC ATIMKIA MALAYSIA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top