• HABARI MPYA

    Monday, November 24, 2014

    TARSIS MASELA UMETHUBUTU LAKINI UMEJIKWAA

    Tarsis Masela anaingia kwenye orodha ya wanamuziki wachache wa muziki wa dansi waliofanikiwa kutoa albam binafsi nje ya bendi wanazozitumikia, tena kubwa zaidi ni kwamba Tarsis amethubutu kufanya hivyo katika kipindi ambacho muziki haununuliki tena, si wa dansi tu bali karibu aina zote za miziki.
    Sasa hivi nyimbo zinatolewa kwaajili kumfanyia msanii au bendi  promosheni ili kupata mafanikio kwenye maonyesho ya ukumbini na ndio maana unaona wasanii wengi wanazigawa bure kupitia mitandao ya kijamii nyimbo zao walizozirekodi kwa gharama kubwa. 

    Mtu anayetoa albam sasa hivi (hasa ya muziki wa dansi) anakuwa na moyo wa kimapinduzi, moyo wa chuma, moyo wa ki-harakati. Kutoa albam huku ukiwa hujui unakwenda kuiuza wapi si jambo la mchezo.
    Ijumaa ya tarehe 21 Novemba 2014 katika ukumbi wa Ten Lounge, Tarsis Masela ambaye ni mwimbaji tegemeo wa Akudo Impact, akaandika historia kwa kuzindua albam yake “Acha Hizo”, ikiwa ni mara yake ya kwanza kufanya hivyo tangu alipoingia Tanzania kutoka Congo DRC zaidi ya miaka saba iliyopita.
    “Acha Hizo” ikashibishwa na nyimbo saba kali ukiwemo “Tabia Mbaya” alomshirikisha Mfalme Mzee Yussuf ambao ulikuwa ndio ‘silaha’ namba moja ya albam hiyo ya Tarsis ambaye ni mwimbaji mzuri mwenye kila kitu – sauti nzuri, tungo nzuri, mvuto mzuri jukwaani pamoja na uwezo mkubwa wa kushambulia jukwaa.
    Maandalizi ya uzinduzi wa albam ya “Acha Hizo” yalikuwa mazuri kuanzia mikutano ya waandishi wa habari pamoja na matangazo ya aina mbali mbali, Tarsis Masela anastahili sifa kwa kila aina ya juhudi aliyofanya.
    Lakini pamoja na mazuri yote ya Tarsis Masela, bado onyesho hilo likazungukwa na mapungufu mengi, nitayataja manne tu.
    Moja: Mahudhurio hayakuwa mazuri sana, hii inatufundisha kuwa si sahihi kwenda kuzindua albam kama huna wimbo uliotawala sana vituo vya radio na televisheni, ni lazima uwe na wimbo ambao ukipigwa ukumbini mashabiki wote wanauimba, kinyume na hapo endelea kuvuta subira – usifanye uzinduzi. 
    Mbili: Kulikuwa na mambo mengi jukwaani ambayo yalifanyika nje ya ratiba. Unapokuwa na onyesho kama hili hakikisha umeipanga vizuri ratiba yako na hutoi kabisa mwanya wa tukio lingine kuteka vichwa vya habari zaidi ya tukio lililowapeleka watu ukumbini.
    Tatu: Washiriki wa albam hawakuonekana jukwaani. Albam ya “Acha Hizo” imeshirikisha wasanii wengi wenye mashabiki kibao – yupo Mzee Yussuf, yupo Lady Jay Dee, yupo pia Chid Benz, bila kumsahau Canal Top – Hawa wote hawakushiriki katika kuimba ‘live’ nyimbo za Tarsis kwa sababu hii na ile, wengine wako nje ya nchi, wengine hawakualikwa, wengine muda uliwatupa mkono, hili lilikuwa kosa la kiufundi, ilipunguza uhalisia wa ladha ya nyimbo zile.
    Nne: Muda ulikuwa ni tatizo – hapa nitaongea sana. Hadi saa 8 usiku bado Tarsis Masela alikuwa hajapanda jukwaani, wimbo wake wa kwanza ulianza kurindima ukumbini saa 9 kasoro usiku, muda ambao show nyingi huwa zinapaswa kuwa zimemalizika, lakini mbaya zaidi hadi saa 9 na robo bado wimbo uliobeba albam “Tabia Mbaya” ulikuwa haujapigwa  hali iliyomfanya Mzee Yussuf akosekane jukwaani wakati wimbo huo ulipopigwa maana aliamua kuondoka ukumbini saa 9 na dakika 20, alichoka kusubiri.
    Hakukuwa na ulazima wowote wa onyesho lile kumalizika saa 10.30 za alfajiri, nilishangaa sana kuona Tarsis Masela anashuka jukwaani saa 10  kwenda kubadili nguo, kabla ya kurejea tena kutumbuiza mbele ya watu wachache sana walioendelea kubaki ukumbini.
    Ni lazima wasanii wetu wafahamu kuwa wapo watu wanaotoka makwao kwenda kwenye maonyesho kufuata wimbo mmoja tu, hivyo kama unaamini wimbo fulani ndiyo silaha yako basi usiucheleweshe hadi alfajiri, upige mapema na kama itabidi kuurudia unaweza kufanya hivyo hiyo alfajiri unayoitaka. Show za dansi zinahudhuriwa zaidi na watu wenye majukumu mengi ya kikazi na kifamilia, wanapaswa kutendewa haki kwa kuwapa ratiba ya kiungwana ili wakapumzike mapema. 
    Maonyesho yetu yanapaswa kuandaliwa kwa mfumo wa pembe tatu – unaanza na rasha rasha, kisha show husika halafu unarudi kwenye rasha rasha …unapoiweka show husika mwishoni kabisa unakuwa kwenye hatari ya kuwakosesha watu wengi tukio hilo na ndivyo ilivyokuwa kwa Tarsis Masela, wengi walichoka na kuondoka ukumbini. 
    Nakumbuka onyesho moja la H- Mbizo na Super Nyamwela pale Travertine Hotel zaidi ya miaka nane iliyopita ambapo mvua zilinyesha saa 8 usiku na kukatisha onyesho wakati Super Nyamwela ndio kwanza akiwa anapanda jukwaani kuzindua albam yake binafisi, mvua ikamtenda - hakufanikiwa kuizindua na hakuzindua tena hata kwa siku za baade, ndiyo maana nasisitiza kuwa na maonyesho ya mfumo wa pembe tatu – mbivu na mbichi zijulikane mapema. Tukutane wiki ijayo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TARSIS MASELA UMETHUBUTU LAKINI UMEJIKWAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top