• HABARI MPYA

    Sunday, November 23, 2014

    HUU KAMA SI UTUMWA TUITE NINI?

    KWA mara nyingine tena, Afrika Mashariki haitakuwa na mwakilishi kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, kufuatia timu zake zote kutolewa mapema.
    Tanzania na Kenya hazikufanikiwa hata kufika hatua ya makundi kuwania fainali hizo, wakati Uganda angalau walipigana hadi siku ya mwisho ya kufuzu.
    The Cranes walishindwa kutimiza ndoto za kucheza tena Fainali za Mataifa ya Afrika tangu ilipocheza mara ya mwisho mwaka 1978, kufuatia kuzidiwa kete na Guinea.
    Ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja, baada ya Nahodha Andy Mwesigwa kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kucheza rafu, Uganda ilichapwa mabao 2-0 na wenyeji Guinea katika mchezo wa Kundi E kufuzu AFCON.

    Mabao ya Guinea yalifungwa na Ibrahima Traore dakika ya 29 na Seydouba Soumah dakika ya 61 kwa penalti baada ya rafu ya Mwesigwa kwenye boksi dakika ya 59.
    Guinea iliyomaliza na pointi 10, imeungana na Ghana iliyoongoza Kundi kwa pointi zake 11 kwenda Equatorial Guinea kwenye fainali za AFCON mapema mwakani.
    Kwa ujumla, katika nchi 11 wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia, Rwanda, Burundi, Eritrea, Sudan Kusini, Djibouti na Somalia hakuna hata moja iliyofuzu. Zanzibar si mwanachama wa FIFA, haichezi mechi za kimataifa, kwa kuwa inachukuliwa kama sehemu ya Tanzania.
    Huu ni mwendelezo wa kudidimia kwa soka ya ukanda wa CECAFA, ambayo mwanzoni mwa historia ya michuano hiyo ilikuwa juu.
    Angalau, katika wanachama wa CECAFA, ni Sudan na Ethiopia ambazo zimeendelea kidogo kututoa kimasomaso kwenye michuano ya kimataifa.
    Sudan wanafanya vizuri hadi kwenye michuano ya klabu, ambako wana nafasi zaidi ya moja kuingiza klabu kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.  
    Uganda wamecheza AFCON tano, 1962 waliposhika nafasi ya nne, 1968,
    1974, 1976 walipokomea Raundi ya Kwanza na hiyo ya kufika fainali 1978.
    Kenya pia wamecheza mara tano, 1972, 1988, 1990, 1992 na 2004 mara zote wakikomea Raundi ya Kwanza, wakati Tanzania imecheza mara moja tu 1980 sawa na Rwanda 2004.
    Sudan wamecheza mara nane fainali hizo, 1957 walipokuwa washindi wa tatu, 1959 washindi wa pili sawa na 1963, 1970 walipochukua ubingwa,
    1972 walipokomea Raundi ya Kwanza sawa na 1976 na 2008 wakati mara ya mwisho walipokwenda AFCON 2012 walifika Robo Fainali.
    Ethiopia walikuwepo kwenye fainali za mwaka jana wakatolewa Raundi ya Kwanza na walicheza pia AFCON za 
    1957 wakawa washindi wa pili, 1959 wakawa wa tatu, 1962 walipokuwa mabingwa, 1963 walipokuwa wa nne, 1965 walikomea Raundi ya Kwanza, 1968 walipokuwa wa nne, 1970 walipokomea Raundi ya Kwanza sawa na 1976,  1982 na 2013.
    Angalau Sudan na Ethiopia zina pa kuhemea, lakini hali mbaya kwa Tanzania, Kenya, Uganda na wanachama wengine wa CECAFA.
    Matatizo ni mengi na siku zote tumekuwa tukiyazungumza, lakini kuyatafutia ufumbuzi limekuwa tatizo kubwa.
    Viongozi wa vyama na mashirikisho ya soka ukanda huu ni tatizo kubwa, wapo madarakani kwa maslahi binafasi zaidi na si maendeleo ya soka.
    Mabadiliko yamekuwa yakifanyika mara kwa mara ya viongozi, lakini bado tatizo limebaki pale pale- na mbaya zaidi, hakuna umoja, upendo wala ushirikiano.
    Ni majungu na fitina tu, hilo ndilo kubwa ambalo ukanda huu wa CECAFA tunaliweza, lakini kuketi chini kutengeneza programu za maendeleo ya soka imekuwa ngumu sana kwetu.
    Watu wanapenda nchi zao, wanapenda timu zao, wanapenda wachezaji wao, lakini wanakatishwa tamaa kwa kiasi kikubwa na viongozi wao.
    Wanalilia mabadiliko, yanatokea, lakini wanaokuja nao, wanarudia yale yale ya waliowatangulia- kwa kweli inakatisha tamaa. AFCON hiyo inakuja, watu wa Afrika Mashariki watapendeza kwa jezi za mataifa mengine na kushinda na kukesha wakiangalia mechi kwenye Televisheni. Huu nao kama si utumwa tuite nini? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HUU KAMA SI UTUMWA TUITE NINI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top