• HABARI MPYA

  Saturday, November 22, 2014

  JAJA ‘ABWAGA MANYANGA’ YANGA SC, MAXIMO AMLETA EMERSON KUZIBA NAFASI YAKE

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Genilson Santana Santos ‘Jaja’ amejiondoa Yanga SC akiwa likizo nchini mwao, Brazil na sasa nafasi yake itazibwa na kiungo mkabaji, Emerson Oliveira Neves Roque, BIN ZUBEIRY imeipata hiyo.
  Jaja amesema ana matatizo ya kifamilia yanayomzuia kurejea Tanzania kufanya kazi- lakini BIN ZUBEIRY inafahamu mshambuliaji huyo ameshindwa kumudu presha ya mashabiki wa klabu ya Jangwani.
  Wapenzi wa Yanga SC hawajaridhishwa na uwezo wa Jaja, aliyeichezea klabu hiyo mechi 11 na kuifungia mabao sita.
  Genilson Santana Santos 'Jaja' anaondoka Yanga SC baada ya kuichezea mechi 11 na kuifungia mabao sita

  Kocha Maximo ambaye yuko likizo Brazil pamoja na Msaidizi wake, Leonardo Leiva na kiungo Andrey Coutinho, amewatumia taarifa Yanga SC kwamba Jaja hatakuja, badala yake anakuja kiungo mkabaji Emerson.
  Emerson mwenye umri wa miaka 24 mzaliwa wa Rio de Janeiro, anakuja Yanga SC akitokea klabu ya 
  Bonsucesso ya mjini humo, ambayo imewahi kucheza Ligi ya Serie B mara mbili, ingawa kwa sasa inacheza ligi ya jimbo la Rio.
  Jaja atakumbukwa kwa mabao yake mawili aliyofunga katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Azam FC, mechi ya Ngao ya Jamii

  Mchezaji huyo anatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Jumanne kwa ajili ya kufanyiwa majaribio na akifuzu atafanyiwa vipimo vya afya, kabla ya kusajiliwa. Wazi mchezaji huyo ana nafasi ya kusajiliwa Yanga SC kwa kuwa analetwa na kocha Maximo.
  Jaja alijiunga na Yanga SC msimu huu, lakini hakuwahi kuwavutia wapenzi wa klabu hiyo, ingawa atakumbukwa kwa mabao yake mawili aliyofunga wakati Yanga SC ikiifunga Azam FC 3-0 katika mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 14, mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: JAJA ‘ABWAGA MANYANGA’ YANGA SC, MAXIMO AMLETA EMERSON KUZIBA NAFASI YAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top