• HABARI MPYA

  Saturday, November 22, 2014

  KASEJA AFUNGUA ‘KESI MPYA’ YA KUONDOKA YANGA SC, FEDHA ZAKE AMELIPWA, ILA SASA...

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  YANGA SC haina deni kwa kipa Juma Kaseja, kama ambavyo yeye mwenyewe anadai, BIN ZUBEIRY imebaini- isipokuwa anataka kuondoka kwa sababu haelewani na kocha wa makipa, Juma Pondamali.
  Novemba 11, mwaka huu kupitia wakili wake, Mbamba & Company Advocates, Kaseja aliwaandikia barua Yanga SC kuwataarifu kuvunja nao Mkataba uliobakiza mwaka mmoja akidai sababu ni kukiukwa kwa masharti yaliyokubaliwa wakati wa kusainiwa Novemba 8, mwaka jana.
  Urafiki wa mashaka; Juma Kaseja kushoto akiwa na kocha wa makipa wa Yanga SC, Juma Pondamali

  Katika barua hiyo, Kaseja amesema wakati wa kusainiwa Mkataba huo ilikubaliwa malipo ya Sh. Milioni 40 yafanyike kwa awamu mbili, ya kwanza, alilipwa Sh. Milioni 20 baada ya kusaini Mkataba huo, na ikakubaliwa fungu lililobaki apatiwe Janauri 15, mwaka huu.
  Akasema kwa sababu malipo ya fedha ndio msingi wa Mkataba wenyewe, kushindwa kulipa fedha hizo kunaondoa uhalali wake, hivyo Mkataba baina yake na Yanga SC umevunjwa rasmi, sasa anaamua kutafuta klabu nyingine.
  Lakini uchunguzi uliofanywa na BIN ZUBEIRY umegundua kwamba, wakati Kaseja anapeleka barua hiyo Yanga SC, tayari fedha zake zilikuwa zimekwishaingizwa kwenye akaunti yake, ingawa ni kweli zilipelekwa nje ya muda wa makubaliano.
  Hata hivyo, baada ya barua, Kaseja alikutana na viongozi wa Yanga SC kuzungumzia mustakabali wake kwa ujumla na kipa huyo akawasilisha madai zaidi, kwamba hana amani ya kufanya kazi katika klabu hiyo kwa mambo mawili.
  Ameyataja mambo hayo ni kutokuwa na maelewano na kocha wa makipa, Juma Pondamali na pia kutoaminika mbele ya baadhi ya viongozi na hadi mashabiki.
  Kaseja amewaomba viongozi wa Yanga wamruhusu aondoke kwa sababu hana amani kwa mambo hayo, ingawa uongozi wa klabu hiyo umeahidi kuwakutanisha na Pondamali kujaribu kumaliza tofauti zao. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KASEJA AFUNGUA ‘KESI MPYA’ YA KUONDOKA YANGA SC, FEDHA ZAKE AMELIPWA, ILA SASA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top