// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); NINI CHA KUFANYA TAIFA STARS ITIMIZE NDOTO ZA KURUDI AFCON, KWENDA KOMBE LA DUNIA? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE NINI CHA KUFANYA TAIFA STARS ITIMIZE NDOTO ZA KURUDI AFCON, KWENDA KOMBE LA DUNIA? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Sunday, August 10, 2014

    NINI CHA KUFANYA TAIFA STARS ITIMIZE NDOTO ZA KURUDI AFCON, KWENDA KOMBE LA DUNIA?

    TANZANIA itasubiri kujaribu tena kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2017, baada ya kukosa nafasi ya kucheza fainali za mwakani Morocco. 
    Hiyo inafuatia kufungwa mabao 2-1 na wenyeji Msumbiji wiki iliyopita katika mchezo wa marudiano, hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Morocco.
    Marefa kutoka nchi jirani, Uganda, wakiongozwa na Dennis Batte walichangia kwa kiasi kikubwa kuitupa nje Tanzania, Taifa Stars baada ya kuwapendelea waziwazi Msumbiji katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Zimpeto mjini Maputo Jumapili iliyopita.

    Na kwa matokeo hayo, Taifa Stars imetolewa katika kwa jumla ya mabao 4-3, baada ya awali kulazimishwa sare ya 2-2 Dar es Salaam, huku Mambas wakienda kuungana na Cape Verde, Niger na Zambia kupigania tiketi ya AFCON ya mwakani Morocco.
    Batte alikataa bao zuri la kichwa la beki Said Mourad aliyeunganisha mpira wa adhabu wa Khamis Mcha ‘Vialli’ baada ya Thomas Ulimwengu kuangushwa dakika ya 17.
    Mshika kibendera nambari moja alimnyooshea kibendera cha kuotea mshambuliaji John Bocco akiwa anakwenda kufunga, wakati alikuwa hajaotea dakika ya 44.
    Bado Batte na wasaidizi wake walitumia ujanja wa kitaaluma kupunguza kasi na mipango ya Stars kusaka mabao- kwa mfano kila wachezaji walipopamiana, mpira ulielekezwa kwa Tanzania- wachezaji wa Msumbiji walikuwa wana maisha mazuri mno mbele ya marefa wa Uganda siku hiyo.
    Baada ya Mganda huyo kupuliza kipyenga cha kumaliza mchezo, wachezaji wa Stars walimfuata kumlalamikia huku wakilia kwa kile walichofanyiwa uwanjani. 
    Wachezaji wa Stars walishindwa kuificha huzuni yao baada ya kuanza kulia uwanjani. 
    Stars ambayo mara ya kwanza na ya mwisho ilicheza AFCON mwaka 1980 enzi hizo bado ikiitwa Kombe la Mataifa Huru ya Afrika, sasa itasubiri mbio za kuwania fainali za michuano hiyo za mwaka 2017 nchini Libya.
    Pamoja na ukweli kwamba mabao yote ya Msumbiji yalikuwa hayana shaka, yalitokana na makosa sugu ya safu yetu ya ulinzi, lakini bado Watanzania wana kila sababu ya kulia na marefa wa Uganda.
    Soka ni mchezo wa makosa- wachezaji wa Tanzania walifanya makosa mawili ambayo Msumbiji waliyatumia kupata mabao, lakini na Tanzania ilitumbukiza mpira nyavuni mara mbili.
    Bao la Mbwana Samatta, refa Batte alishindwa kulikataa, lakini bao zuri la kichwa la Mourad alilikataa. Bado Bocco alifanikiwa kuwazidi kasi mabeki wa Msumbiji akawa anakwenda kufunga kabla ya kunyooshewa kibendera cha kuotea.
    Msumbiji walichezeshwa kwa haki Dar es Salaam na wakapata sare ya 2-2, lakini hali haikuwa hivyo walipokuwa nyumbani. Walibebwa.
    Refa Batte ndiye ambaye pia aliwachezesha Msumbiji katika mchezo wa hatua ya kwanza ya mchujo dhidi ya Sudan Kusini- na haijulikani kuna siri gani baina yake na CAF na nchi hiyo, hata akapangiwa kuwachezesha Mambas mfululizo.
    Inafahamika soka ya Afrika imetawaliwa na rushwa- lakini hatuwezi kumshutumu moja kwa moja, Batte kama alihongwa, labda yalikuwa makosa ya kibinadamu, lakini ambayo yamewaumiza Watanzania.
    Tanzania ndiyo nchi iliyopitia katika mtihani mgumu kuliko ndugu zao wa Afrika Mashariki katika kampeni hizi za awali za AFCON, ikumbukwe hatua ya kwanza waliitoa Zimbabwe.
    Na wakati Stars wanatolewa kwa mbinde na Msumbiji hatua ya pili na ya mwisho ya mchujo, jirani zao Uganda waliitoa timu dhaifu ya Mauritania, huku Kenya wakikwama kwa vibonde Lesotho, wakiwa na nyota wao wa Ulaya, McDonald Mariga, Dennis Oliech na Victor Wanyama.
    Bila shaka Watanzania wangetamani ratiba ya Kenya au Uganda iwe yao- kwa imani kwamba wangefuzu, tena kiulaini. 
    Kocha Mholanzi, Mart Nooij aliwasili mwishoni mwa Aprili kuja kurithi mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen ambaye naye alishindwa kuipa mafanikio Tanzania.
    Hali ilifikia pabaya mno Stars chini ya Kim, kiasi cha kufungwa nyumbani na ugenini na timu kama Uganda, jambo ambalo lilisababisha timu hiyo ipoteze mvuto kabisa mbele ya wananchi.
    Kwa kipindi kifupi cha Nooij kuwa na timu, kuna mabadiliko kiasi fulani yanaonekana- ambayo yanatoa matumaini kwamba mtaalamu huyu wa Kiholanzi, akipewa muda zaidi anaweza kuifikisha mbali timu yetu.
    Kwanza Nooij alikuwa anafanya kazi na wachezaji ambao hawakuwa chaguo lake, kwani alifika nchini wakati ambao Ligi Kuu imemalizika hivyo hakupata fursa ya kuteua wachezaji kwa kuwaona wakicheza.
    Siku anafika, Aprili 26 alikuta Stars inacheza mchezo wa kirafiki na Burundi ikafungwa 3-0, ikiundwa na wachezaji wasio na uzoefu waliopatikana katika mpango wa maboresho ya timu hiyo.
    Wazo la mpango wa maboresho lilikuja baada ya kuona wachezaji wanaoonekana bora katika ligi yetu kwa sasa wanashindwa kuisaidia timu, hivyo TFF chini ya rais wake, Jamal Malinzi ikajaribu kutafuta njia mbadala.    
    Kweli wachezaji wa maboresho walionyesha wana vipaji, lakini kwa kukosa uzoefu walipoteza sifa za kuwa wachezaji wa timu ya taifa na Nooij alikuwa sahihi kuomba aitiwe wazoefu.
    Ndipo wakarejeshwa wachezaji waliokuwa Stars chini ya Kim Poulsen ambao walikwishawafanya Watanzania wapoteze mapenzi na timu yao ya taifa. 
    Nooij akawandaa wachezaji hao hao na akafanikiwa kuitoa Zimbabwe, timu ngumu na iliyo juu yetu kiuwezo, kabla ya kukwama kwa Mambas.
    Bado timu yetu haijaimarika kiasi cha kuridhisha, lakini siku hadi siku chini ya Nooij mabadiliko yanaonekana. Ni imani kwamba, Ligi Kuu itakapoanza na Nooij atakaposhuhudia wachezaji tofauti, kwanza atafanya mabadiliko ya kikosi kwa kuita wachezaji chaguo lake kabla ya kuanza upya kutengeneza timu.
    Katika wachezaji 11 wanaokuwa uwanjani Stars wakati wote, unaweza kuona wachezaji wasiozidi watano tu wenye ubora kweli wa kimataifa, lakini wengine wanakuwapo kwenye timu sababu labda hakuna wengine.
    Hivyo kuna mtihani wa kwanza wa kupandisha viwango vya wachezaji- tupate watu aina ya Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza TP Mazembe ya DRC, au hata Amri Kiemba wa Simba SC, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga na Shomary Kapombe wa Azam FC.
    Jambo kubwa na zuri kwa sasa ni kuona wachezaji wetu wanakwenda kucheza nchi zilizopiga hatua kidogo kisoka kama hao akina Samatta, ili wapandishe viwango vyao.
    Lakini na Ligi Kuu ya Bara pia inahitaji kuboreshwa ili iwe ya ushindani zaidi- kuwafanya wachezaji wawe bora. Walimu wa kigeni wanaoajiriwa na baadhi ya klabu za hapa, watusaidie kupandisha viwango vya wachezaji wetu na si kutaka wepesi wa kununuliwa wachezaji wa kigeni.
    Kwa miaka miwili mfululizo mfungaji bora wa Ligi Kuu anakuwa mgeni, wachezaji wanaong’ara wanakuwa wageni- tutarajie wachezaji bora wa Taifa Stars watatoka wapi?   
    Dhahiri tuna kazi nzito ya kufanya kuhakikisha tunakuwa na timu bora ya taifa itakayotimiza ndoto za Watanzania kuiona Taifa Stars inacheza fainali za mashindano makubwa. Lazima tuyatazame kwa mapana marefu matatizo ya timu yetu na namna ya kuyatatua pia. 
    Kweli, marefa ‘wananyonga’ na walituumiza sana mbele ya Mambas mjini Maputo- lakini dawa ni kuwa na timu bora, wachezaji bora zaidi ambao hata waamuzi wakifanya hila, inakuwa bado na uwezo wa kufanya vizuri.
    Kila mmoja anajua, Stars ilitolewa Dar es Salaam baada ya kulazimishwa sare nyumbani, makosa ya aina hiyo hayapaswi kurudiwa- mechi za nyumbani ni za kushinda.
    Kufikiria kuhonga marefa ni hatari na kuitendea dhambi soka- jambo bora ni kufanyia kazi mapungufu yetu siku hadi siku bila kukata tamaa na kama tutaendelea hivyo, naamini iko siku tutarudi AFCON. Iko siku tutakwenda Kombe la Dunia. Mungu ibariki Tanzania. Ibariki timu yetu ya taifa. Amin. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NINI CHA KUFANYA TAIFA STARS ITIMIZE NDOTO ZA KURUDI AFCON, KWENDA KOMBE LA DUNIA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top