• HABARI MPYA

  Sunday, August 24, 2014

  CECAFA WAKIENDELEA NA UBISHI WAO, KOMBE LA KAGAME LITAZIDI KUPOTEZA HADHI YAKE

  MICHUANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame inafikia tamati leo mjini Kigali, Rwanda kwa mchezo wa fainali baina ya wenyeji APR na El Merreikh ya Sudan.
  Awali michuano hiyo ilikuwa ikifanyika mwanzoni tu mwa mwaka, Januari, lakini kwa zaidi ya miaka mitano sasa, michuano hiyo imehama kutoka kufanyika mwanzoni mwa mwaka hadi Julai na Agosti.
  Mara ya mwisho michuano hiyo kufanyika mwanzoni mwa mwaka, ilikuwa mwaka 2003 mjini Kampala, Uganda kati ya Januari na Februari, SC Villa ikiifunga 1-0 Simba SC ya Tanzania katika fainali bao pekee la Mkenya, Vincent Tendwa dakika ya 79, akimalizia krosi ya Mtanzania Shaaban Kisiga ‘Malone’.

  Siwezi kuisahau fainali moja tamu ndani ya Uwanja wa Mandela, Namboole, ambayo makocha Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ akiwa Villa na Mkenya James Sianga walishikana kutaka kupigana.
  Kikosi kilichopipa ubingwa SC Villa kilikuwa; Postnet Omwony, David Kateregga, Sula Walusimbi akatoka akaingia mfungaji wa bao Vincent Tendwa, Robert Tumusiime, Timothy Batabaire, Emmanuel Balyejusa, Phillip Ssozi, Edgar Watson, Ekuchu Kasongo akatoka akaingia Samuel Mubiru, Ismail Kigozi aliyempisha mtoa pasi ya bao Kisiga na Nestroy Kizito.
  Simba SC katika moja ya miaka yake mizuri, kikosi chake kiliundwa na Juma Kaseja, Said Sued, Ramadhan Wasso, Victor Costa, Boniface Pawasa, Suleiman Matola, Steven Mapunda ‘Garrincha’ aliyempisha Edibily Lunyamila dakika ya 76, Christopher Alex aliyempisha Emmanuel Gabriel dakika ya 50, Athumani Machupa aliyempisha Jumanne ‘Shengo’ Tondola dakika ya 65, Madaraka Selemani na Ulimboka Mwakigwe.
  Baada ya mwaka huo, michuano ikaanza kulegalega na kuanza kuhama kalenda taratibu hadi sasa imefikia kufanyika Agosti.
  Rwanda walipewa uenyeji wa michuano  ya mwaka uliofuata ambayo ilitakiwa kuanza Desemba 27 mwaka 2003 hadi Januari 13, mwaka 2004.
  Lakini Shirikisho la Soka la Rwanda (FERWAFA) likaomba kuandaa kuanzia Machi 28  na Aprili 14,  ili michuano hiyo iende sambamba na maazimisho ya miaka 10 ya mauaji ya kimbari yaliyotokea mwaka 1994.
  Hata hivyo, matokeo yake mashindano yakasogezwa tena mbele  na kafanyika kuanzia Aprili 25 hadi Mei 9 wenyeji APR wakitwaa taji la kwanza kwa kuifunga mabai 3-1 Ulinzi Stars ya Kenya.
  APR ilitoka nyuma  kwa bao la Sammy Simiyu dakika ya 10 na kupata mabao matatu kupitia kwa Olivier Karekezi dakika ya 13 na Jimmy Gatete dakika ya 49 kwa penalti na 70.
  Mwaka uliofuata michuano ilikuja Tanzania na ilitakiwa kufanyika kati ya Februari 13 na 28, lakini matokeo yake ikafanyika kati ya Aprili 23 na Mei 8.
  SC Villa iliivua ubingwa APR kwa kuichapa mabao 3-0 kwenye fainali- wafungaji Robert Ssentongo dakika ya 44 na Mkenya, Ben Mwalala aliyeibuka mfungaji bora mawili dakika ya 52 na 90.
  Michuano ya mwaka 2006 ilikuwa ifanyike Uganda, lakini wakachemsha  na ikahamishiwa Dar es Salaam, ambalo ilifanyika kati ya Mei 13 na 28, Polisi ya Uganda ikiifunga 2-1 Moro United Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mbele ya Rais Jakaya Kikwete.
  Mambo yameendelea hivyo na sasa limekuwa ni jambo la kawaida kupokea michuano hiyo katikati ya mwaka kuelekea mwisho , yaani kuanzia Julai na Agosti.
  Inaaminika haikuwa dhamira ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kuifikisha michuano hiyo katika kipindi hicho, bali dharula ilisababisha yote.
  Lakini pamoja na ukweli huo, CECAFA wanaonekana wamekwishanogewa na kufanya michuano hii katikati ya mwaka.
  Na inawezekana ni kwa sababu wamesahau faida za kufanya mashindano haya mwanzoni mwa mwaka.
  Nitawakumbusha; wakati mashindano yanafanyika Januari yalisaidia mno timu za ukanda huu kupata maandalizi kabla ya kuanza michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.
  Yalisaidia timu zilizotoka kushiriki mashindano hayo ziingie na moto kwenye ligi za nchini kwao.
  Mabinga halisi wa Ligi za nchi wanachama wa CECAFA walipatikana kwa sababu  kipindi cha mwanzoni mwa mwaka hawakuwa kwenye mashindano mengine.
  Kwa kufanya mashindano haya katikati ya mwaka; tumeshuhudia baadhi ya nchi zikishindwa kutuma mabingwa wake kwa sababu mbalimbali.
  El Hilal ya Sudan ilikuwa bado kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Ethiopia nao walituma timu isiyo ya Ligi Kuu, Adama City.
  Yanga SC ilishindwa kwenda Rwanda kwa sababu haikuwa imejiandaa na badala yake ilitaka kupeleka kikosi cha vijana na kuchanganya wakongwe wachache.
  CECAFA wakakataa na Azam FC ikapewa nafasi, ingawa nayo ilikurupushwa tu, haikuwa imejiandaa.
  Wazi, kama michuano hii itarudi kufanyika Januari timu zote stahili zitashiriki kama zamani na msisimko utaongezeka zaidi.
  Vigumu kuelewa kwa nini CECAFA wameweka nta masikioni mwao juu ya hili- wakati mambo yako wazi kwamba sasa wanafanya mashindano haya bila tija kwa klabu.
  Iwapo CECAFA itaendelea kupuuzia mpango wa kuirudisha michuao hii Januari, basi tutarajie hadhi yake ikishuka zaidi. Wasalam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CECAFA WAKIENDELEA NA UBISHI WAO, KOMBE LA KAGAME LITAZIDI KUPOTEZA HADHI YAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top