• HABARI MPYA

  Ijumaa, Agosti 29, 2014

  MAXIMO ASEMA YANGA SC ITAANZA LIGI KUU NA MOTO, ‘AWAPANDISHIA MIZUKA’ AZAM FC MECHI YA NGAO

  Na Samira Said, DAR ES SALAAM
  KOCHA wa Yanga SC, Mbrazil, Marcio Maximo amesema kwamba watauanza msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kishindo. 
  Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo, Jangwani, Dar es Salaam, Maximo amesema kwamba imani hiyo inatokana na maandalizi mazuri waliyoyapata walipokuwa Zanzibar.
  Maximo amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi katika mechi za timu hiyo ili kuishangilia timu.
  Hata hivyo, Maximo amesema timu yake imepangiwa ratiba ngumu katika mechi za mwanzoni, lakini watapambana kufanya vizuri.
  Maximo akizungumza na Waandishi wa Habari Jangwani leo


  Amesema watacheza mechi mbili za kirafiki Jumatano na Jumapili na kwamba ataendelea na utamaduni wa kutoa nafasi kwa wachezaji wote kucheza.
  Maximo amesema ana matumaini makubwa mechi hizo mbili zitawasaidia kujiimarisha kuelekea msimu mpya, wakianza na mchezo wa Ngao ya Jamii, dhidi ya mabingwa, Azam FC Septemba 13, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Ligi Kuu inatarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu, mabingwa watetezi wakianza na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Septemba 20, mwaka huu, wakati Yanga SC waliomaliza nafasi ya pili wataanza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro siku hiyo.
  Washindi wa tatu, Mbeya City wataanza na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Sokoine, Mbeya Septemba 20 na washindi wa nne, Simba SC wataanza na Coastal Union ya Tanga Septemba 21, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mechi nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu zitakuwa kati ya Stand United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MAXIMO ASEMA YANGA SC ITAANZA LIGI KUU NA MOTO, ‘AWAPANDISHIA MIZUKA’ AZAM FC MECHI YA NGAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top