• HABARI MPYA

  Friday, August 29, 2014

  SAKATA LA OKWI; YANGA SC WATAKA SIMBA NA MCHEZAKJI MWENEYWE WOTE WAFUNGIWE, WAIPA TFF SIKU SABA KUCHUKUA HATUA, VINGINEVYO KESI FIFA HADI CAS…WATAKA FIDIA PIA YA SH MILIONI 900

  Na Samira Said, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imekana kumpa barua Emmanuel Okwi ya kuvunja naye Mkataba na imesema mshambuliaji huyo Mganda, amewahadaa Simba SC ambao wameingia mkenge.
  Na sasa, Yanga SC imeandika barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikiiomba ifanye mambo mawili- 1- imfungie Okwi kucheza soka na 2- iifungie Simba SC.
  Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari mchana wa leo, makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji amesema kwamba anaipa TFF siku saba kutekeleza hayo.  Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari leo. Kushoto Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga

  Manji amesema, iwapo TFF itashindwa kutekeleza hayo ndani ya siku hizo saba, wao watahamia Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambako kama hawatafanikiwa pia, watahamia Mahama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS).
  Manji amesema leo asubuhi wametuma malalamiko yao kimaandishi TFF na pia wanamdai Okwi fidia ya dola za Kimarekani 500,000 (Sh. Milioni 900) kutokana na kuvunja mkataba na wao.
  “Tunataka Okwi afungiwe kucheza soka na Simba ifungiwe kutokana na kumsainisha Okwi. Tumeipa TFF siku saba ifanyie kazi malalamiko yetu,” amesema Manji.
  Mwenyekiti huyo amesema kwamba, kabla ya jana katika malalamiko ya awali waliyotuma TFF, walitaka Okwi awalipe dola 200,000 (zaidi ya Sh. Milioni 340,000), lakini baada ya Simba kutangaza imemsajili jana, dau limepanda.
  Manji amesema kwamba Yanga haina ubaya na Simba, bali watani wao hao wa jadi, wamefanya vibaya kumsainisha mchezaji huyo bila kuwasiliana nao. 
  “Simba SC walipaswa kuja kutuuliza kabla ya kumchukua Okwi, na wala sisi hatuna ugomvi na Simba, endapo watafungiwa au kushushwa daraja wasilie na Yussuf,”amesema.
  Amesema Yanga haitatetereka kwa kuondoka kwa Okwi, shida ni kwamba taratibu hazikufuatwa. “Yanga imeachana na walimu na wachezaji mbalimbali kama Freddy Mbuna, Nsajigwa Shadrack kwa amani. Na nilisema mapema katika mkutano wa Juni, kwamba Okwi kama hatarudi, tutasajili wachezaji wengine wazuri, nimesajili Coutinho (Andrey) na Jaja (Geilson Santana),”amesema Manji.
  Jana Okwi ametangaza kurejea Simba SC kwa mkataba huru wa muda, akida Yanga SC imempa barua ya kusitisha mkataba naye pamoja na kumshitaki TFF.
  Okwi alisema ameamua kuomba kuichezea Simba SC kipindi hiki ambacho ana matatizo na Yanga SC ili kulinda kipaji chake, kwa kuwa hata FIFA haitaki mchezaji akae bila kucheza.
  “Sasa wakati Yanga wanaendelea na kesi yao, mimi ninaomba nichezee Simba SC ili kulinda kipaji changu. Nimewaandikia barua TFF na FIFA pia na nina matumaini usajili wangu utaidhinishwa, kwa sababu mimi si tatizo katika hili,”amesema.
  Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe alisema kwamba wamemsaini mchezaji huyo baada ya kupitia kwa kina suala lake na Yanga SC na kugundua haki ipo upande wa mchezaji.
  “Baada ya kulipitia suala lake na Yanga kwa undani kabisa na vielelezo ambavyo mchezaji mwenyewe ametupatia, tumejiridhisha tuko sahihi kumsaini ili acheze mpira kunusuru kipaji chake kipindi hiki ambacho ana matatizo na Yanga SC,”alisema Poppe.  
  Okwi akiwa na Hans Poppe jana wakati anarejea Simba SC

  Okwi aliichezea Simba SC tangu mwaka 2009 kabla ya Januari mwaka jana kuuzwa kwa dola za Kimarekani 300,000 (Sh. Milioni 500) Etoile du Sahel ya Tunisia.
  Etoile haikulipa fedha hizo Simba SC na baadaye ikaingia kwenye mgogoro na Okwi, aliyedai hakulipwa pia mishahara yake kwa miezi mitatu.
  Okwi akawafungulia Etoile kesi FIFA na akaomba wakati mgogoro wao unaendelea, aruhusiwe kuchezea timu yoyote kulinda kipaji chake, ndipo akajiunga na SC Villa ya kwao.
  Akiwa SC Villa ndipo aliposaini Yanga SC Desemba mwaka jana na pamoja na mapingamizi yaliyoanzia ndani, na baadaye klabu yake, Etoile- lakini Okwi aliidhinishwa kuichezea timu hiyo ya Jangwani.
  Okwi aliichezea Yanga SC mechi 11 na kuifungia mabao matano- lakini kuelekea mechi tano za mwisho za Ligi Kuu msimu uliopita akaingia kwenye mgogoro na klabu hiyo.
  Okwi alisusa kushinikiza amaliziwe fedha zake za usajili na mgogoro wao umeendelea huku mchezaji huyo akiwa amesusa tangu Machi, miezi minne tu baadaye tangu asajiliwe.
  Vikao kadhaa vimekwishafanyika baina ya Okwi na Yanga SC tangu hapo kutafuta suluhu ya suala hilo na kikao cha mwisho jana baina ya mchezaji huyo na Manji matokeo yake ni nyota huyo kurejea Msimbazi.
  Kuhusu deni lao la dola 300,000 kumuuza mchezaji huyo Etoile, Poppe amesema haihusiani kabisa na usajili wake huu wa sasa. “Ile kesi yetu ya madai ya fedha zetu kule FIFA ilikwishamalizika na vielelezo vyote vilipelekwa, bado kutolewa hukumu tu,” amesema. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAKATA LA OKWI; YANGA SC WATAKA SIMBA NA MCHEZAKJI MWENEYWE WOTE WAFUNGIWE, WAIPA TFF SIKU SABA KUCHUKUA HATUA, VINGINEVYO KESI FIFA HADI CAS…WATAKA FIDIA PIA YA SH MILIONI 900 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top