• HABARI MPYA

  Sunday, August 24, 2014

  KAREMBEU ATAKA TIMU YA KUKOCHI TANZANIA, ASEMA ANASUBIRI OFA NONO AJE KUPIGA MZIGO IWE KLABU AU TIMU YA TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Christian Karembeu amesema kwamba yupo tayari kuja kufundisha soka Tanzania, iwapo atapata maslahi mazuri.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Karembeu alisema kwamba kama ofa nzuri itapatikana anaweza kuja kufanya kazi ya ukocha Tanzania.
  “Ninaweza, kwa nini hapana, kama nitapata ofa nzuri nitakuja, ninaipenda Afrika,”alisema Karembeu baada ya kuulizwa kama akipata ofa ya kufundisha Tanzania atakubali. 
  Niko tayari; Karembeu kulia akizungumza na Mtendaji Mkuu wa BIN ZUBEIRY Blog, Mahmoud Zubeiry jana Uwanja wa Taifa 
  Karembeu aliyezaliwa Desemba 3, mwaka 1970 mjini Lifou, New Caledonia ambaye kwa sasa ni Mshauri wa Mipango (Strategic Advisor) wa Olympiacos ya Ugiriki alisema hayo baada ya mechi baina ya magwiji wa Real Madirid ya Hispania na Tanzania.
  Karembeu aliiongoza Real Madrid kushinda 3-1 dhidi ya wachezaji nyota wa zamani wa Tanzania, mabao yote yakifungwa na Reuben de La Red.      
  Rasta huyo alikonga nyoyo za maelfu ya mashabiki waliojumuika na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete katika mchezo huo kwa soka yake maridadi.
  Karembeu katika mchezo wa jana
  Karembeu akiwalimiana na watoto jan Taifa
  Na baada ya mechi, Karembeu alitumia fursa ya kwenda kupeana mikono na Rais JK kwa kutoa simu yake kujipiga ‘selfie’ na mkuu huyo wa nchi ya Afrika Mashariki.  
  Ezi zake Karembeu alichezea timu za Nantes kati ya 1990 hadi 1995, Sampdoria kati ya 1995 na 1997, Real Madrid kati ya 1997 hadi 2000, Middlesbrough 2000 na 2001, Olympiacos 2001 na 2004, Servette 2004 na 2005 Bastia 2005 na 2006, timu zote akicheza jumla ya mechi 425 na kufunga mabao 24.
  Alikuwemo kwenye kikosi cha Ufaransa kilichotwaa Kombe la Dunia nyumbani mwaka 1998- na tangu 1992 hadi 2002 alipostaafu alichezea timu hiyo mechi 53 na kuifungia bao moja.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAREMBEU ATAKA TIMU YA KUKOCHI TANZANIA, ASEMA ANASUBIRI OFA NONO AJE KUPIGA MZIGO IWE KLABU AU TIMU YA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top