• HABARI MPYA

  Wednesday, August 27, 2014

  MAGURI AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO SIMBA SC IKIUA 2-0 AMAAN

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  MSHAMBULIAJI Elias Maguri amefunga bao lake la kwanza Simba SC ikishinda mabao 2-0 dhidi ya wenyeji Mafunzo jioni hii Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika mchezo wa kirafiki.
  Mchezaji huyo aliyesajiliwa kutoka Ruvu Shooting ya Pwani msimu huu, alifunga bao hilo la kwanza katika mchezo huo, dakika ya 60 baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Mrundi Amisi Tambwe.
  Maguri alifunga bao zuri, baada ya kupokea pasi ya Said Ndemla, akamlamcha chenga hadi chini beki wa Mafunzo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Khalid Mahadhi. 
  Elias Maguri amefunga bao lake la kwanza Simba SC leo
  Winga Haroun Chanongo aliifungia Simba SC bao la pili dakika ya 71 baada ya kuuvunja mtego wa kuotea wa mabeki wa Mafunzo, kufuatia pasi ya kutanguliziwa na Maguri.
  Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kukiwa hakuna bao na mchezo ulikuwa wa mashambulizi ya pande zote mbili, ingawa Simba SC ndiyo waliotengeneza nafasi nyingi zaidi.
  Peke yake Amri Kiemba alikaribia mara mbili kufunga na mara zote mpira ukatoka nje sentimita chache, wakati Ramadhani Singano ‘Messi’ naye alipoteza nafasi moja ya wazi.
  Jaku Joma Jaku alifumua shuti kali akiwa ndani ya boksi la Simba SC, lakini kipa Ivo Mapunda akadaka kwa ustadi mkubwa.
  Maguri alimlamba chenga hadi chini beki wa Mafunzo kabla ya kufunga

  Kiungo Mrundi, Pierre Kwizera aliumia dakika ya 35 na akatibiwa kwa dakika mbili kabla ya kurejea uwanjani, lakini kocha Mzambia, Patrick Phiri akampumzisha dakika ya 42, nafasi yake akichukua Said Ndemla.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda/Hussein Sharrif ‘Cassilas’ dk80, Miraj Adam/William Lucian ‘Gallas’ dk80, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’/Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ dk80, Joram Mgeveke/Donald Mosoti dk80, Joseph Owino/Hussein Butoyi dk80, Pierre Kwizera/Said Ndemla dk42, Haroun Chanongo/Uhuru Suleiman dk80, Amri Kiemba/Abdallah Seseme dk65, Amisi Tambwe/Elias Maguri dk46, Shaaban Kisiga ‘Malone’/Ibrahim Hajibu dk80 na Ramadhani Singano ‘Messi’/Twaha Ibrahim ‘Messi’.
  Mafunzo; Khalid Mahadhi, Haji Abdi Hassan, Ali Hassan ‘Larson’, Said Yussuf Mkadam, Juma Othman Mmanga, Said Mussa Shaaban, Mohammed Abdulrahim, Amour Abdullah Bhai, Rashid Abdallah Karihe, Jaku Joma Jaku na Ally Othman Mmanga. 
  Kiungo Shaaban Kisiga akimuacha chini beki wa Mafunzo
  Pierre Kwizera aliumia leo, lakini akaendelea kwa dakika kadhaa kabla ya kutoka 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAGURI AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO SIMBA SC IKIUA 2-0 AMAAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top