• HABARI MPYA

    Friday, August 22, 2014

    LUNYAMILA ACHEMSHA MAZOEZI YA MINZIRO, AOMBA POO MWENYEWE TAIFA, ASEMA…

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WINGA wa zamani machachari wa kimataifa wa Tanzania, Edibily Jonas Lunyamila jana alilazimika kutoka nje, baada ya kuhisi misuli inamuuma, kufuatia mazoezi makali ya fiziki ya kocha Freddy Felix Minziro.
    Kikosi maalum cha wachezaji waliovuma katika soka ya Tanzania miaka kadhaa iliyopita, jana kilikuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa mazoezi kujiandaa na mechi dhidi ya magwiji wa Real Madrid ya Hispania kesho kwenye Uwanja huo.
    Na makocha watatu, Charles Boniface Mkwasa, Minziro na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ walipeana awamu za kuwanoa wachezaji wanaounda timu hiyo inayoitwa Tanzania Eleven.
    Alianza Julio katika mazoezi ya kujenga pumzi, kwa kukimbia, akafuatia Minziro kwenye mazoezi ya fiziki na hapo ndipo Lunyamila alipochemka.
    Alichemsha; Edibily Lunyamila akiwa mazoezini jana Taifa

    Baada ya kurusuhwa rushwa na kunyooshwa viungo, Lunyamila alisema anasikia misuli inavuta akaomba kwenda kupumzika, akiwa hoi.
    “Misuli inavuta nimeona bora nikae nje kidogo,”alisema Lunyamila na alipoulizwa kama ataweza kucheza kesho, alisema; “Ndiyo maana nimeomba kupumzika ili niweze kucheza Jumamosi”alisema winga huyo wa zamani wa Yanga.  
    Mechi kali ya kihistoria inatarajiwa kupigwa Taifa baina ya magwiji wa Tanzania na Magalacito wa Real Madrid na mwanasoka bora wa zamani wa dunia, Luis Figo ameahidi burudani nzuri ya soka kesho Uwanja wa Taifa.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana huu katika hoteli ya Southern Sun, Dar es Salaam, mshindi huyo wa Ballon d’Or mwaka 2000, aliyestaafu Mei 31 mwaka 2009, amesema kwamba Watanzania watafurahia kazi yake uwanjani kesho.
    Figo aliyepiga tuzo mbili mfululizo mwaka 2000, Mwanasoka Bora Ulaya na Dunia, amewaomba wapenzi wa soka Tanzania kujitokeza kwa wingi kesho kushuhudia burudani.
    “Ni mara yangu ya kwanza kuja Tanzania, nimekwishatembea nchi kadhaa Afrika, nimefurahi kuja hapa, naipenda Afrika. Natarajia mchezo mzuri kesho, hata kwa wapinzani wetu pia, kitu muhimu ni kwamba FIFA imefurahia tukio hili,”alisema Figo.
    Kutoka kushoto Abubakar Kombo, Emmanuel Gabriel na Lunyamila
    Lunyamila akiwa benchi baada ya kuchemsha mazoezi ya Minziro

    Kwa upande wake, mwanasoka bora wa Oceania mara mbili 1995 na 1998, Christian Karembeu aliyeshinda Kombe la Dunia na Ufaransa mwaka 1998, amesema kwamba atampa pasi nyingi kesho Figo afanye vitu vyake.

    Beki wa zamani wa kimataifa wa Hispania, Fernando Sanz Duran ni miongoni mwa wanasoka watatu waliowika Real Madrid muongo uliopita waliofika jana usiku, ambaye pia alikuwepo kwenye mkutano wa leo.
    “Nimefurahi kuja Tanzania, ni mara yangu ya kwanza, Watanzania watarajie burudani nzuri kutoka kwetu na wapinzani wetu,”alisema Sanz huku akimgusa begani, kocha Msaidizi wa Magwiji wa Tanzania, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LUNYAMILA ACHEMSHA MAZOEZI YA MINZIRO, AOMBA POO MWENYEWE TAIFA, ASEMA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top