• HABARI MPYA

  Jumatano, Agosti 27, 2014

  AZAM FC WAANZA KUIPASHIA YANGA SC KESHO CHAMAZI, KIMBEMBE KITAKUWA TAIFA SEPTEMBA 13

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MABINGWA wa Bara, Azam FC wanatarajiwa kuanza tena mazoezi kesho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam baada ya kurejea kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mjini Kigali, Rwanda.
  Katibu wa Azam FC, Nassor Idrissa Mohammed ‘Father’ ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba wachezaji wote wataanza mazoezi kesho, kasoro wale ambao wameitwa timu ya taifa.
  Father amesema kwamba wachezaji wawili, Aishi Manula na Kevin Friday japokuwa hawapo kwenye kikosi cha Taifa Stars, wao wamepewa mapumziko zaidi- hivyo si lazima waanze kesho.
  Azam FC wanatarajiwa kuanza mazoezi kesho kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga SC Septemba 13, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

  Aidha, Father alisema kwamba Simba SC waliomba mchezo wa kirafiki na wao wikiendi hii, lakini imeshindikana kwa sababu kocha Joseph Marius Omog amesema hawezi kuwa na mechi baada ya mazoezi ya siku mbili.
  “Mwalimu amesema mchezo wanaotaka Simba SC labda wiki ijayo, kwa sababu hawezi kufanya mazoezi Alhamsi na Ijumaa halafu baada ya hapo awe na mechi, ngumu,”amesema.
  Mcamreoon huyo, Omog ameifikisha Azam FC Robo Fainali ya Kombe la Kagame mjini Kigali kabla ya kutolewa na El Merreikh ya Sudan, iliyoibuka bingwa wa michuano hiyo mwaka huu. 
  Wachezaji wa Azam waliotwa na kocha Mholanzi Mart Nooij kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Morocco mjini Marakech Septemba 5, mwaka huu ni kipa Mwadini Ali, mabeki ni Said Morad, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, viungo Erasto Nyoni, Himid Mao, Salum Abubakar na mshambuliaji John Bocco. 
  Wataingia kambini Agosti 31, mwaka huu mchana katika hoteli ya Accomondia mjini Dar es Salaam.
  Azam FC inatarajiwa kukutana na wapinzani wao katika mbio za ubingwa msimu uliopita, Yanga SC kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, Septemba 13, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Aidha, mabingwa hao wataanza kutetea taji lao la Ligi Kuu kwa kumenyana na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Septemba 20, mwaka huu, wakati Yanga SC waliomaliza nafasi ya pili wataanza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro siku hiyo.
  Washindi wa tatu, Mbeya City wataanza na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Sokoine, Mbeya Septemba 20 na washindi wa nne, Simba SC wataanza na Coastal Union ya Tanga Septemba 21, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mechi nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu zitakuwa kati ya Stand United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC WAANZA KUIPASHIA YANGA SC KESHO CHAMAZI, KIMBEMBE KITAKUWA TAIFA SEPTEMBA 13 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top