• HABARI MPYA

  Wednesday, August 27, 2014

  NANI ALIJUA SIKU MOJA MAREKANI ITATAWALIWA NA MWEUSI, NANI ANABISHA TANZANIA INAWEZA KUANDAA AFCON?

  TANZANIA imetuma barua makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mjini Cairo, Misri kuomba kuandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2017, kufuatia Libya kujitoa.
  Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema wiki hii kwamba wana uwezo na wako tayari kuwa wenyeji wa fainali hizo- ndiyo maana wameomba.
  Libya imeamua kujitoa kutokana na vurugu za kisiasa zinazoendelea nchini humo- hivyo kuhofia mazingira ya kiusalama.
  Awali, Libya ilipewa uenyeji wa fainali za mwaka 2013, lakini ikajitoa kwa sababu kama hizo na Afrika Kusini ikapewa nafasi hiyo- huku makubaliano yakifikiwa wao wataandaa AFCON ya mwaka 2017.

  Jumamosi ikatangazwa tena, Libya imejitoa baada ya viongozi wa nchi hiyo kukutana na Rais wa CAF, Issa Hayatou.
  CAF ikasema jitihada za kumsaka mbadala wa Libya zinaanza mara moja- maana yake kujitokeza kwa Tanzania ni ahueni kwao.
  Mara baada ya tamko hilo la Rais wa TFF, midajala ilifuatia kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, baadhi wakibeza wazo hilo.
  Kwa waliopinga, wengi hawakuwa na hoja na zaidi ilionekana waliwasilisha hisia za chuki dhidi ya Malinzi au nafsi za kujikatia tamaa.
  Nimeikiliza na kupitia maoni ya wengi wanaopinga sehemu tofauti- ili kujua hoja zao ni zipi- lakini kwa bahati mbaya hawakuwa na hoja za msingi.
  Kwa mtazamo wa haraka, wengi waliopinga ama ni chuki zao binafsi au wengine ni wale waliokata tamaa ambao hawaamini Tanzania inaweza chochote. 
  Mtu mmoja alisema, baada ya kukosa nafasi ya kucheza AFCON, Malinzi ameona njia ya mkato ni hiyo, kuwa mwenyeji kwa kuwa tutashiriki moja kwa moja.
  Yaani ni vituko tu- tangu ameingia madarakani, Malinzi amepigania AFCON moja tu ya mwakani Morocco ambayo tumeshindwa kwa sababu ambazo wengi wetu tuliona.
  Vijana walimwaga machozi Uwanja wa Zimpeto baada ya refa Mganda, Dennis Batte kuwanyonga Maputo dhidi ya Msumbiji. 
  Tulishindwa kufuzu kwa miaka yote tangu tulipofuzu mara ya kwanza na ya mwisho 1980, shirikisho likiwa na viongozi wengine, si Malinzi. 
  Watanzania wengi ni watu wa kukatishana tamaa, mtu kwa uvivu wake kwa kuwa ameshindwa yeye, basi atataka kumkatisha tamaa na mwingine.
  Watanzania wengi wa siku hizi tumekuwa watu ambao hatupendani, hatutakiani mema na wala hatuna uzalendo na taifa letu- na haya kwa kiasi kikubwa yanaturudisha nyuma kimaendeleo.
  Kwa umri wake Malinzi ni mtu mzima, mwenye uzoefu wa kutosha na desturi za Watanzania wenzake walio wengi- nataka nimkumbushe kitu kimoja katika utawala wake; “If you have no critics, you will have no success,”.
  Maneno haya aliwahi kusema, mwanaharahati wa haki za binadamu, Malcom Little maarufu Malcom X, au El Hajj Malik El Shabazz (sasa marehemu) baada ya kusilimu na kwenda Hijja. 
  Alikuwa akimaanisha kwamba, kama hutapambana na changamoto ya kukosolewa, hautaweza kufikia mafanikio.
  Ndiyo, mtu anapokukosoa na wakati uko sahihi, ni kipimo cha kujiamini kwako juu ya jambo husika. Maana yake kama unaamini fikra zako, hautayumbishwa.
  Nimekuwa nikifuatilia AFCON kwa muda sasa kuanzia aina ya nchi ambazo zinapewa uenyeji na kadhalika na ninaweza kuwa miongoni mwa wale wanaoamini Tanzania inaweza kwa sasa kuwa mwenyeji wa fainali hizo.
  Hoja ya kwamba hatuna viwanja ni ovyo- Tanzania ina viwanja visivyopugua vitano vyenye sifa, ingawa vingine vitahitaji marekebisho madogo.
  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hakuna shaka una sifa zote kwa mechi ya ufunguzi na fainali, wakati CCM Kirumba mjini Mwanza, Amaan Zanzibar na Sheikh Amri Abeid Arusha vitahitaji marakebisho kidogo.   
  Ukarabati wa Uwanja wa Uhuru umekamilika na bila shaka kwa pamoja na viwanja vingine vilivyotajwa, zoezi linawezekana.
  Mwingine akaibuka na hoja ya hoteli, jamani nchi hii sasa kuna shaka juu ya hoteli zenye hadhi katika miji yetu mikuu? Hadi Manzese kuna mahoteli ya kifahari siku hizi.
  Ndiyo maana nasema wengine waliotoa maoni yao, wamejikatia tamaa, kiasi kwamba hawana imani na nchi yao kama inaweza chochote.
  Miundombinu katika miji yote hiyo mikuu, Mwanza, Arusha, Zanzibar na Dar es Slaam kwa sasa ipo vizuri. Tunaweza.
  Lakini pia baada ya kukubaliwa kuna muda wa maandalizi na sapoti pia kutoka CAF kwenyewe kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa kabla ya michuano yenyewe.
  Mtoa hoja mmoja alihoji, timu tunayo? Hilo liliniingia akilini- kwamba ili tufurahie uenyeji wa mashindano, lazima tuhakikishe tunaandaa timu ya kushindana.
  Wachezaji tunao, lakini kwa kiwango cha ushindani wa michuano kama AFCON watahitaji maandalizi madhubuti. Na katika hilo, muda upo.
  Itakapowadia AFCON ya 2017 ndipo wachezaji kama Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Aishi Manula, Shomary Kapombe, Simon Msuva, Himid Mao, Said Ndemla na chipukizi wengine watakuwa wamekomaa haswa.
  Sioni wapi tutafeli kama kutakuwa na mipango na Watanzania wote tukaunganisha nguvu zetu, bila kujali itikadi zetu kuhakikisha hilo linafakiwa kwa heshima ya nchi yetu.
  Kwanza kuomba uenyeji, ukipatikana mipango ya maandalizi ya timu na uenyeji wenyewe wa mashindano vitafuatia.
  Nani alijua siku moja Marekani itatawaliwa na Rais mweusi na nani anabisha Tanzania inaweza kuandaa Fainali za Mataifa ya Afrika? Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NANI ALIJUA SIKU MOJA MAREKANI ITATAWALIWA NA MWEUSI, NANI ANABISHA TANZANIA INAWEZA KUANDAA AFCON? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top