• HABARI MPYA

  Jumatatu, Agosti 25, 2014

  TANZANIA KUANDAA KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA BAADA YA LIBYA KUJITOA

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  TANZANIA itaomba kuandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2017, kufuatia Libya kujitoa.
  Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba wana uwezo na wako tayari kuwa wenyeji wa fainali hizo- hivyo wataomba.
  “Tutaomba kuwa wenyeji wa AFCON ya 2017 kuziba pengo la Libya, tuko tayari na tuna uwezo, tunatarajia sapoti kubwa ya Serikali na wadau wengine wa Tanzania katika hili,”amesema Malinzi.
  Libya imeamua kujitoa kutokana na vurugu za kisiasa zinazoendelea nchini humo- hivyo kuhofia mazingira ya kiusalama.
  Burudani inakuja; Rais wa TFF, Jamal Malinzi kushoto akiwa na Rais wa CAF, Issa Hayatou

  Awali, Libya ilipewa uenyeji wa fainali za mwaka 2013, lakini ikajitoa kwa sababu kama hizo na Afrika Kusini ikapewa nafasi hiyo- huku makubaliano yakifikiwa wao wataandaa AFCON ya mwaka 2017.
  Jumamosi ikatangazwa tena, Libya imejitoa baada ya viongozi wa nchi hiyo kukutana na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Issa Hayatou.
  CAF ikasema jitihada za kumsaka mbadala wa Libya zinaanza mara moja- maana yake kujitokeza kwa Tanzania ni ahueni kwao.
  Kwa sasa, Tanzania inaweza kabisa kuwa mwenyeji wa fainali hizo kwa kuwa ina viwanja visivyopugua vitatu vyenye sifa, ingawa vingine vitahitaji marekebisho madogo.
  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hakuna shaka una sifa zote, wakati CCM Kirumba mjini Mwanza na Sheikh Amri Abeid Arusha vitahitaji marakebisho kidogo.   
  Iwapo Tanzania itafanikiwa kupata uenyeji wa fainali za mwaka 2017, itakuwa imefuzu moja kwa moja kucheza michuano hiyo bila kupitia kwenye hatua ya mchujo.
  Na hiyo itakuwa mara ya pili kihistoria kushiriki AFCON baada ya 1980 mjini Lagos, Nigeria wakati huo bado michuano hiyo ikiitwa Kombe la Mataifa ya huru ya Afrika.
  Tanzania ilipangwa Kundi A pamoja na wenyeji Nigeria, Ivory Coast na Misri na ikashika mkia. Ilifungwa 3-0 na Ngeria, 2-1 na Misri na kutoka sare ya 1-1 na Ivory Coast.  
  Yapo matumaini makubwa Tanzania ikafanikiwa kupewa yenyeji wa michuano hiyo mwaka 2017, kutokana na uhusiano mzuri baina ya Hayatou na rais wa sasa wa TFF, Malinzi. Kwa ujumla, FIFA na CAF zina imani kubwa na utawala wa Malinzi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TANZANIA KUANDAA KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA BAADA YA LIBYA KUJITOA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top