• HABARI MPYA

  Monday, August 25, 2014

  MAZEMBE YATOKA SARE NA AS VITA MCHEZO WA MWISHO MAKUNDI LIGI YA MABINGWA, SASA KUKUTANA NA ES SETIF NUSU FAINALI

  Na Mwandishi Wetu, KINSHASA
  BAADA ya sare ya bila kufungana na wapinzani wao wakubwa, AS Vita jana mjini Kinshasa, TP Mazembe imemaliza kileleni mwa Kundi A katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
  AS Vita ilicheza bila ya mchezaji wake aliyesimamishwa kwa kuichezea Rwanda akiwa ni Mkongo, Dady Birori.
  Mchezaji huyo, wiki iliyopita alisimamishwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kukutwa na hatia ya kutumia majina mawili tofauti katika pasipoti mbili.

  Sakata la Birori limeiponza Rwanda kuenguliwa katika hatua ya makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco.
  Timu hizo mbili za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimemaliza na pointi 11 kila moja, lakini TP Mazembe imejituliza kileleni kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
  Na sasa, Mazembe itakutana na ES Setif ya Algeria katika Nusu Fainali, wakati AS Vita itakutana na CS Sfaxien ya Tunisia, mechi za kwanza zikichezwa kati ya Septemba 19 na 21 na marudiano kati ya Septemba 26 na 28.
  Mazembe yenye washambuliaji wawili wa Tanzania, Mbwana Samatta aliyeanza jana na Thomas Ulimwengu aliyetokea benchi, itaanzia ugenini, wakati AS Vita itaanzia nyumbani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAZEMBE YATOKA SARE NA AS VITA MCHEZO WA MWISHO MAKUNDI LIGI YA MABINGWA, SASA KUKUTANA NA ES SETIF NUSU FAINALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top