• HABARI MPYA

  Jumamosi, Agosti 30, 2014

  SIMBA SC YAIFUMUA 5-0 KMKM, OKWI ASUGUA BENCHI

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  SIMBA SC imewafunga mabingwa wa Zanzibar, KMKM mabao 5-0 katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  KMKM inayofundishwa na Ally Bushiri ‘Bush’ ambayo Jumatano wiki hii ilifungwa 2-0 na Yanga SC, leo iligeuzwa asusa na Wekundu wa Msimbazi.
  Simba SC ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza mabao 4-0, yaliyotiwa kimiani na Amisi Tambwe mawili, Amri Kiemba na Shaaban Kisiga ‘Malone’ moja kila mmoja.
  Amisi Tambwe na Ramadhano Singano 'Messi' kulia wakishangilia usiku huu Amaan

  Amri Kiemba ndiye aliyefungua karamu ya mabao ya Simba SC hii leo, dakika ya tatu ya mchezo baada ya kupewa pasi nzuri na kiungo Mrundi, Pierre Kwizera na kuwatoka wachezaji wawili wa KMKM kabla ya kufumua shuti kali lililogonga mwamba wa ndani wa lango.
  Amisi Tambwe akafuatia dakika ya 14 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Salim Amour kufuatia yeye mwenyewe kupiga mkwaju wa penalti, baada ya kiungo, Haroun Chanongo kuangushwa kwenye boksi.
  Tambwe tena akafunga bao la tatu dakika ya 23 akimalizia krosi maridadi ya Ramadhani Singano ‘Messi’ kabla ya Kisiga kufunga la nne dakika ya 37, kufuatia kazi nzuri ya Kiemba.
  Beki wa Simba SC, Issa Rashid 'Baba Ubaya' akimtoka mchezaji wa KMKM usiku huu
  Wazito; Kutoka kulia Musley Ruwey, Hans Poppe na Salim Abdallah 'Try Again' 

  Kipindi  ha pili, kocha Mzambia, Patrick Phiri alibadilisha kikosi kizima akimuacha Nahodha Jopseph Owino pekee na dakika ya 60 Elias Maguri akahitimisha karamu ya mabao kwa bao safi la tano.
  Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi aliyetangaza juzi kurejea Simba SC kutoka kwa mahasimu, Yanga SC usiku huu alikuwepo, lakini alibaki benchi muda wote wa mchezo.
  Okwi katikati akiwa na Mosoti kulia na Butoyi kushoto
  Viongozi wa Simba SC wakiongozwa Makamu wa Rais, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe, Kassim Dewji, Musley Ruwey, Mohammed Nassor ‘Steven Seagal’, Crescentius Magori, Said Tuliy na wengineo walikuwepo kushuhudia mchezo huo.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda/Hussein Sharrif ‘Cassilas’ dk46/Peter Manyika dk84, Miraj Adam/Abdi Banda dk46/Nassor Mssoud ‘Cholo’dk84, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’/William Lucian ‘Gallas’ dk46/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk84, Joram Mgeveke/Hassan Isihaka dk46, Joseph Owino, Pierre Kwizera/Abdallah Seseme dk46, Haroun Chanongo/Twaha Ibrahim ‘Messi’ dk46, Amri Kiemba/Ibrahim Hajibu dk46, Amisi Tambwe/Elias Maguri dk46, Shaaban Kisiga ‘Malone’/Awadh Juma dk46 na Ramadhani Singano ‘Messi’/Uhuru Suleiman dk46.
  KMKM; Salim Amour, Pandu Hajji, Faki Hamad/Makame Hajji dk30, Juma Rashid/Nassor Ali dk30, Halfan Khamisi/Mudrik Muhibu dk30, Moka Shaaban, Ame Khamis, Abdi Kassim ‘Babbi’, Haji Simba/Kassim Nemshi dk30, Maulid Ibrahim na Khamis Ali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAIFUMUA 5-0 KMKM, OKWI ASUGUA BENCHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top