• HABARI MPYA

  Jumapili, Agosti 31, 2014

  OWINO NAHODHA MPYA SIMBA SC, KISIGA MSAIDIZI WAKE, CHOLLO AVULIWA BEJI BAADA YA KUPOTEZA NAMBA ‘FIRST ELEVEN’

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  BEKI Mganda, Joseph Owino ameteuliwa kuwa Nahodha wa Simba SC, nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Nassor Masoud ‘Chollo’ ambaye amepoteza namba mbele ya kocha mpya, Mzambia Patrick Phiri.  
  Phiri alimuanzisha katika mchezo mmoja tu wa kirafiki Chollo dhidi ya Kilimani, ambao ndio ulikuwa wa kwanza kwa timu hiyo katika kambi yake ya Zanzibar, lakini tangu hapo amekuwa akimpanga kinda Miraj Adam. 
  Baada ya Miraj kufanya vizuri katika mechi dhidi ya Mafunzo na KMKM, Phiri ameamua kuteua viongozi wapya wa wachezaji wenzao, Owino akiwa Nahodha Mkuu na Shaaban Kisiga ‘Malone’ akiteuliwa kuwa Nahodha Msaidizi. 
  Bosi wa wachezaji; Joseph Owino ameteuliwa kuwa Nahodha mpya Simba SC
  Owino akiwatambulisha wachezaji wa Simba SC kwa mgeni rasmi jana Uwanja wa Amaan

  Simba SC imeweka kambi visiwani Zanzibar kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, unaotarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu.
  Pamoja na kufanya mazoezi, Simba SC imecheza mechi tatu za kujipima nguvu hadi sasa, dhidi ya Kilimani waliyoshinda 2-1, Mafunzo 2-0 na KMKM 5-0, zote Uwanja wa Amaan.
  Ligi Kuu inatarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu, mabingwa watetezi wakianza na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Septemba 20, mwaka huu, wakati Yanga SC waliomaliza nafasi ya pili wataanza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro siku hiyo.
  Washindi wa tatu, Mbeya City wataanza na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Sokoine, Mbeya Septemba 20 na washindi wa nne, Simba SC wataanza na Coastal Union ya Tanga Septemba 21, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mechi nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu zitakuwa kati ya Stand United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  Naodha Msaidizi; Shaaban Kisiga 'Melone' amerudi na mguu mzuri Simba SC
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: OWINO NAHODHA MPYA SIMBA SC, KISIGA MSAIDIZI WAKE, CHOLLO AVULIWA BEJI BAADA YA KUPOTEZA NAMBA ‘FIRST ELEVEN’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top