• HABARI MPYA

    Sunday, July 13, 2014

    STRAIKA WA AZAM ATUA RUVU KWA MKOPO

    Na Renatus Mahima, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Ruvu Shooting ya Pwani imemsajili kwa mkopo wa miezi sita mshambuliaji Seif Rashid Abdallah wa Azam FC.
    Masau Bwire, msemaji wa Ruvu Shooting, amethibitisha usajili wa mshambuliaji huyo katika mahojiano na BIN ZUBEIRY muda mfupi uliopita.
    Kabla ya kusajiliwa Azam dirisha dogo la msimu wa 2012/13 kutoka Ruvu Shooting, straika huyo alikuwa ameitumikia klabu hiyo ya maafande wa Pwani kwa mafanikio makubwa.
    Wakati mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo msimu wa 2012/13 unamalizika Abdallah alikuwa amefungia Ruvu Shooting magoli sita, mawili nyuma ya Didier Kavumbagu (wa Yanga kipindi hicho) na Kipre Tchetche wa Azam.
    Seif Abdallah kulia alishindwa kupata namba kikosi cha kwanza Azam FC

    “Kocha wetu (Mkenya Tom Olaba) amesema amefurahishwa na usajili wa mshambuliaji huyo katika kikosi chake ambacho anaamini sasa safu ya upachikaji magoli imeimarika na itatisha zaidi kwa timu vigogo nchini,” amesema Bwire.
    Mchezaji huyo amekuwa wa sita kusajiliwa na maafande hao kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili kesho, wengine wakiwa ni Zuberi Dabi (Kagera Sugar), Chagu Chagula (Mzinga ya Burundi), Juma Mpakala, Salvatory Ntebe na Yusuph Nguya (wote kutoka Mtibwa Sugar).
    Timu hiyo ya Kanali Charles Mbuge iko kambini Mlandizi, Pwani tangu Juni 9 kujiandaa kwa msimu ujao wa VPL utakaoanza Septemba 20.
    Seif Abdallah mara chache alikuwa akiingia kutokea benchi Azam FC
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STRAIKA WA AZAM ATUA RUVU KWA MKOPO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top