• HABARI MPYA

    Wednesday, March 21, 2012

    TFF ISIFANYE KOSA KUIPA TBL TAIFA STARS

    
    Kikosi cha Stars kulia kikiwa Denmark kucheza na wenyeji, kilipelekwa na SBL, waliokuwa wadhamini wa kwanza wa timu hiyo kihistoria.
    MKATABA wa udhamini wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) umemalizika tangu Desemba mwaka jana na sasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lipo kwenye mchakato wa ama kuongeza mkataba na SBL, au kuingia mkataba mpya na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL). SBL walianza kuidhamini Stars mwaka 2006, ikiwa haina na haijawahi kuwa na mdhamini. Katika kipindi hicho, SBL ilitekeleza vema mkataba wake wa udhamini na timu hiyo na kuonekana dhahiri kuvuka mipaka katika kuhakikisha timu inakuwa na maandalizi mazuri na kujenga hamasa ya mashabiki kurejesha mapenzi kwa timu yao ya taifa.
    Kwa kiasi kikubwa, Tanzania walibaki mashabiki wawili tu wa soka, mmoja wa Simba na mwingine wa Yanga, lakini timu ya taifa haikuwa ikipendwa kabisa.
    Mechi za timu ya taifa zilikuwa hazivutii mashabiki kabisa na hakuna kingine kilichosababisha hali hiyo zaidi ya kushuka kwa kiwango cha timu yenyewe na uongozi mbovu uliokosa dira ya maendeleo kwa soka ya nchi hii.
    Wengi wanaamini hata SBL walijitokeza kuisaidia timu ya taifa, ili kuunga mkono jitihada za rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alianza kwa kutimiza ahadi yake ya kuipatia timu hiyo kocha wa kigeni, kwa kumleta Mbrazil Marcio Maximo.
    Ndiyo kwa sababu wakati huo timu hiyo ilikuwa haiuziki kwa yoyote na hata TBL hawakuwa wakiitaka wakati huo.
    SBL imefanya mambo mengi yenye kuonekana wakati wake ikiidhamini Stars tangu 2006 hadi mwaka jana Desemba mkataba ulipoisha.
    Iligharamia kambi za muda mrefu kuanzia nyumbani na ugenini, ili kuhakikisha timu yetu inajengwa vema na kuwa ya ushindani.
    Huwezi kusahau kambi za mafunzo Bulyanhulu mkoani Shinyanga, baadaye Brazil na nchi za Scandinavia.
    Chini ya Maximo kwa udhamini wa SBL tulishuhudia timu yetu imekuwa ya ushindani tena na kukaribia kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2008 nchini Ghana kama si kufungwa na Msumbiji katika mechi ya mwisho nyumbani.
    Hadhi ya timu ya taifa ilipanda na tulishuhudia timu kubwa kama Brazil na Ivory Coast zikipokea mwaliko wa kuja kucheza nasi mechi za kirafiki hapa.
    Matunda ya udhamini wa SBL ni timu yetu kufuzu kucheza Fainali za kwanza za CHAN  nchini Ivory Coast na kwa mara ya kwanza Watanzania waliwashuhudia wachezaji wao kwenye luninga wakicheza michuano mikubwa ya Afrika.
    Kweli, baadaye timu yetu iliporomoka na zaidi ilitokana na matatizo ya ndani ya shirikisho, nidhamu za wachezaji na ‘ujuaji’ wetu Waandishi na wachambuzi wa Tanzania uliotugharimu tukampoteza kocha mzuri, Marcio Maximo.
    Lakini bado hata katika wakati mgumu, wakati wa kuporomoka kwa timu ya taifa, bado SBL iliendelea kuwa bega kwa bega na timu ya taifa- hata baada ya Maximo kuondoka na hatimaye mwaka juzi timu ya Bara ikatwaa Kombe la Challenge baada ya miaka 15.
    Tanzania Bara, ambayo huundwa na asilimia 90 ya wachezaji wa Taifa Stars inayoundwa kwa mseto wa wachezaji wa Bara na visiwani Zanzibar, ambayo kwenye Challenge hushiriki kama nchi kamili, ilitwaa Kombe hilo mara ya mwisho mwaka 1994 nchini Kenya.
    Kombe la Challenge lilirejea Bara chini ya kocha mpya, Mdenmark Jan Borge Poulsen, lakini kutokana na msingi mzuri wa ujenzi wa timu uliofanywa na Maximo.
    SBL wamekuwa wavumilivu na kuendelea kuidhamini Stars bila ya kujali matokeo mabaya, ambayo yalisababisha mashabiki waanze kuizomea timu yao.
    Lakini baada ya mkataba wao kufikia tamati Desemba, hadi sasa hawajafikia mwafaka wa mkataba mpya na TFF, kwa sababu bodi hiyo ya soka nchini imepandisha dau la udhamini kutoka Sh. Bilioni 1.2 hadi Bilioni 3.6, ambayo ni zaidi ya asilimia 300.
    Wakati huo huo, kuna habari kwamba TBL iko tayari kuipokea SBL katika kuidhamini timu hiyo kwa dau la Sh. Bilioni 3.6 kwa mwaka.
    Vema. Hizi ni habari njema kwa timu yetu. Lakini tunapaswa kuzingatia kwamba, TBL tayari ni wadhamini wakuu wa Kombe la Taifa, ni wadhamini wakuu wa klabu za Simba na Yanga.
    Kuwapa na timu ya taifa pia, maana yake sasa wao ndio watakaokuwa wamebeba mustakabali mzima wa soka ya nchi hii, jambo ambalo kwa mtazamo wangu naona ni hatari.
    TBL kama kampuni, ambayo ina maamuzi yake binafsi ambayo nje ya misingi ya sheria- hayawezi kuwa na upinzani wala kipingamizi chochote.
    Nini namaanisha, leo TBL inataka kuingia mkataba wa udhamini wa timu ya taifa, ikiwa tayari inadhamini Kombe la Taifa na klabu za Simba na Yanga kwa sababu viongozi wa sasa wa kampuni hiyo wanaridhia hilo.
    Lakini ni hatari ikitokea akaletwa kiongozi mwingine pale TBL kutoka Afrika Kusini- ambaye atakuwa hana mapenzi na soka. Anaweza kuamua mara moja, mikataba inayoendelea ikifikia tamati na iwe basi na hakuna anayeweza kupingana nao.
    Lakini soka ya Tanzania itaingia kwenye wakati mgumu sana- kumpoteza mtu ambaye alikuwa nguzo muhimu kama mdhamini wa klabu za Simba na Yanga, Kombe la Taifa na timu ya taifa kwa wakati mmoja.
    Historia ndio inaleta wasiwasi huu. Mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania Bara ilikuwa inadhaminiwa na TBL, lakini katika hatua za mwishoni mwa ligi hiyo, kampuni ilijitoa kwa sababu ambayo sisiti kusema ndogo tu.
    Aliyekuwa Waziri wa Michezo wakati huo, Profesa Juma Athumani Kapuya kwa utashi wake aliongeza timu mbili katika hatua ya mwisho na kuwa nane badala ya sita, ambazo wakati huo FAT ilikubaliana na TBL.
    TBL ilikerwa na hilo na ikasitisha udhamini wake mara moja na mwaka huo, ingawa timu ziliitangaza bia ya Safari Lager kwa robo tatu ya msimu, lakini hazikupata chochote, pole zaidi kwa mabingwa wa mwaka huo, Simba SC ambao walikosa zawadi.
    Wakubwa walisema tu, TBL ya sasa iko chini ya Wazungu na hawataki mambo yetu ya Kiswahili, hivyo kwa uswahili wa Kapuya kuongeza timu katika hatua ya mwisho ya ligi hiyo wao wakajitoa na ligi ikabaki yatima.
    Najaribu kutafakari, uswahili alioufanya Kapuya wakati huo, kama angeufanya katika kipindi ambacho TBL ingekuwa mdhamini wa Ligi Kuu, Kombe la Taifa na timu ya taifa, soka ya nchi hii ingekumbwa na janga kubwa kiasi gani?
    Kweli, TBL wanakuja na dau kubwa kuliko SBL, lakini ipo haja ya TFF kutafakari mara mbili faida na athari za kuikabidhi soka yetu yote kwa TBL.
    Sitaki kuzungumzia malumbano ya mara ya kwanza na klabu za Simba na Yanga juu ya utekelezaji wa mikataba yao ya udhamini, ikiwemo kelele za kucheleweshewa mishahara au kutopewa mabasi mapya makubwa waliyoahidiwa tangu wasaini mikataba mipya mwaka jana- ila tu nawaasa TFF, wawe makini na maamuzi yao. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF ISIFANYE KOSA KUIPA TBL TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top