• HABARI MPYA

  Saturday, October 06, 2018

  SIMBA SC YAANZA HARATATI ZA KUTETEA UBINGWA, YAIPIGA AFRICAN LYON 2-1 NA KUJIVUTA JUU

  Na Saada Salmin, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imeamsha makali yake baada ya kuichapa African Lyon ya Dar es Salaam mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam usiku wa leo.
  Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 14 baada ya kucheza mechi saba, ikijivuta hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Azam FC pointi 15 za mechi saba, Singida United pointi 16 mechi tisa na Mtibwa Sugar pointi 17 mechi tisa.
  Ushindi wa leo wa Simba SC umetokana na mabao ya kiungo mzalendo, Shiza Ramachani Kichuya kipindi cha kwanza na mshambuliaji wake Mganda, Emmanuel Okwi kipindi cha pili, wakati bao la Lyon limefungwa na Awadh Juma dakika ya 62.
  Kichuya ambaye ameporomoka kiasi cha kuachwa timu ya taifa, leo aliamsha makali yake kwa kufunga bao la kwanza mapema tu dakika ya nane akimalizia krosi ya beki wa kulia, Shomari Kapombe.

  Wa Uganda wote; Emmanuel Okwi (kushoto) akipongezwa na Meddie Kagere (kulia) baada ya kufunga bao la pili. Anayewafuta kushoto ni Shiza Kichuya, mfungaji wa bao la kwanza 

  Okwi hakuwa na bahati kipindi cha kwanza baada ya kupoteza nafasi nzuri dakika ya 11 kufuatia kumdakisha kipa wa Lyon, Tonny Charles baada ya pasi nzuri ya Kapombe.
  Mnyarwanda aliyezaliwa Uganda, Meddie Kagere naye hakuwa na siku nzuri kwa mara nyingine leo, baada ya mchomo wake kuokolewa na beki Ismail Gambo wa Lyon dakika ya 18 ukiwa unalekea nyavuni.
  Kassim Mdoe wa African Lyon akaikosesha bao timu yake dakika ya 28 baada ya kupiga shuti hafifu lililodakwa kwa urahisi na kipa namba moja wa taifa na Simba SC, Aishi Manula.
  Mara mbili, Okwi akafanikiwa kuziwahi vizuri krosi za Kapombe kuunganisha kwa kichwa dakika 29 na 33 lakini bahati mabaya mipira ikaenda nje.
  Hatimaye ukawadia wakati wa Okwi ‘kufuta gundu’ kwa kufunga bao lake la kwanza la msimu katika Ligi Kuu, akiifungia Simba SC bao la pili dakika ya 47 kwa kichwa kufuatia krosi nzuri ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
  Okwi akataka kuwaadhibu tena Lyon ambao leo walikosa huduma ya mkongwe wao, Haruna Moshi ‘Boban’ aliyekuwa anatumikia adhabu ya kadi ya njano, lakini shuti lake la mbali dakika ya 54 likatoka nje.
  African Lyon wakapata bao lao pekee dakika ya 61 kupitia kwa mshambuliaji wake, Awadhi Juma aliyemtungua ‘Tanzania One’, Aishi Manula kwa shuti la mbali.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, James Kotei, Cletus Chama/Haruna Niyonzima dk67, Shiza Kichuya/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk68, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi/Said Ndemla dk87.
  African Lyon: Tonny Charles, Daudi Mbweni, Baraka Jaffar, Agustino Samson, Emmanuel Simwanza, Said Mtikila/Adam Omar Soba dk70, Awadhi Juma, Ismail Gambo/Kassim Kilungo dk90, Kassim Mdoe, Victor da Coasta na Hamisi Thabiti/Khalfan Mbarouk dk26.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAANZA HARATATI ZA KUTETEA UBINGWA, YAIPIGA AFRICAN LYON 2-1 NA KUJIVUTA JUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top