• HABARI MPYA

  Monday, October 08, 2018

  NGOMA AANZA MOTO WA MABAO AZAM FC YAICHAPA 2-0 COASTAL UNION NA KUPANDA KILELENI LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  USHINDI wa mabao 2-0 ilioupata Azam FC dhidi ya Coastal Union usiku huu, umeifanya kukamata usukani wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL).
  Azam FC sasa inafikisha pointi 18 baada ya kucheza mechi nane, ikishinda tano na sare tatu, mbele ya Mtibwa Sugar yenye pointi 17 mechi tisa, Yanga SC pointi 16 mechi sita, Singida United pointi 16 mechi tisa na mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 14 za mechi saba.
  Alikuwa ni mshambuliaji Donald Ngoma, aliyeifyungulia ukurasa wa mabao Azam FC akifunga dakika ya 28 akitumia pasi safi ya kiungo Mudathir Yahya.
  Bao hilo linamfanya Ngoma, kufungua akaunti ya mabao Azam FC tokea asajiliwe msimu huu ikiwa ni mechi yake ya tatu kuichezea Azam FC baada ya kutoka kwenye majeraha ya muda mrefu ya goti.

  Donald Ngoma akishangilia baada ya kuifungia Azam FC bao la kwanza leo
  Donald Ngoma akimiliki mpira kwa ustadi mkubwa mbele ya mchezaji wa Coastal Union

  Kabla ya bao hilo, dakika ya 12 Ngoma alikaribia kuipatia bao jingine Azam FC baada ya kufanya kazi nzuri ya kuwahadaa mabeki wa Coastal na kupiga shuti lililopanguliwa wa kipa Hussein Shariff ‘Casillas’ na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
  Dakika ya 17 winga wa Azam FC, Enock Atta, aliyeonekana kurejea vema alifanya kazi ziada ya kuwatoka mabeki wa Coastal na kupiga shuti la chini lililogonga mwamba wa pembeni kabla ya mabeki kuondoa hatari hiyo.
  Azam FC iliendelea na kasi yake ya kutaka kupata mabao zaidi, lakini safu ya ulinzi ya Coastal ilisimama vema kuondoa hatari zote na kufanya kipindi cha kwanza kuisha kwa uongozi wa bao hilo kwa mabingwa hao.
  Kipindi cha pili Azam FC iliendelea na kasi yake na kutengeneza nafasi kadhaa lakini wachezaji wa Coastal Union waliendelea kulinda vema lango kwa kuondoa hatari zote.
  Mabadiliko ya benchi la ufundi la Azam FC kumuingiza mshambuliaji Danny Lyanga dakika ya 65 na kutoka Ngoma, yaliongeza kasi zaidi eneo la ushambuliaji la timu hiyo.
  Dakika ya 70 Lyanga aliifunga timu yake ya zamani kwa bao safi la umbali wa takribani mita 21 akitumia vema uzembe wa mebeki wa Coastal walioiokoa vibaya krosi iliyochongwa na beki David Mwantika.
  Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kwa siku mbili kabla ya kurejea tena mazoezini Alhamisi hii kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya African Lyon utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Oktoba 19 mwaka huu.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razack Abalora, David Mwantika, Hassan Mwasapili, Abdallah Kheri, Agrey Moris, Mudathir Yahya, Joseph Mahundi/Idd Kipagwile dk84, Salum Abubakar 'Sure Boy', Donald Ngoma/Danny Lyanga dk65, Yahya Zayed, Enock Atta -Agyei/Ramadhan Singano 'Messi' dk75.
  Coastal Union; Hussein Shariff 'Cassilas', Adam Mohammed, Adeyum Saleh, Ibrahim Amme, Bakar Mwamnyeto, Hassan Ally, Issa Abushehe/Haji Ugando dk58, Mohammed Twaha/Prosper Mushi dk84, Mtenje Albino, Deogratius Anthony/Moses Kitandu dk84 na Ayub Lyanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGOMA AANZA MOTO WA MABAO AZAM FC YAICHAPA 2-0 COASTAL UNION NA KUPANDA KILELENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top