• HABARI MPYA

    Sunday, June 10, 2018

    YAKUBU AANZA KUJIFUA AZAM FC, NGOMA NJE WIKI TISA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    DAKTARI Mkuu wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa amesema kwamba beki majeruhi wa muda mrefu, Mghana Yakubu Mohammed aliyevunjika mguu na kukosa sehemu kubwa ya mechi za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ameruhusiwa kuanza mazoezi tangu Juni1, mwaka huu.
    Mwankemwa ameyasema hayo Jumamosi katika Mkutano na Waandishi wa Habari kuzungumzia maendeleo ya wachezaji mbalimbali wa Azam FC majeruhi.
    Alisema Amoah, aliyefanyiwa upasuaji wa goti nchini Afrika Kusini atarejea dimbani baaada ya miezi tisa kupita tokea siku aliyoumia Februari mwaka huu, akimaanisha kuwa atarejea Oktoba mwaka huu.

    Beki Mghana wa Azam FC, Yakubu Mohammed ameanza mazoezi Azam FC tangu Juni 1, mwaka huu

    “Mchezaji mwingine ni kijana wetu Stanslaus Ladislaus tuliyempelekea kwa mkopo African Lyon, tulimfanyia uchunguzi katika Hospitali ya Hi Tech naye amekutwa na tatizo la kuchanika mtulinga wa kati kwenye goti lake la mguu wa kulia na tunafanya taratibu hivi sasa za kumpeleka Afrika Kusini,” alisema.
    Kuhusu mshambuliaji kutoka Yanga, Mzimbabwe Donald Ngoma, Daktari huyo amesema kwamba atarejea dimbani Agosti 11 mwaka huu tayari kuanza kuitumikia timu hiyo kwa mechi za ushindani.
    Ngoma ni usajili mpya wa Azam FC kwa ajili ya msimu ujao na sasa ni wazi atakuwa fiti kucheza mechi za msimu ujao wa ligi akiwa na sura nyingine mpya, kama kiungo Tafadzwa Kutinyu, ambaye usajili wake umeshakamilika akitokea Singida United aliyoichezea msimu uliopita. 
    Baada ya kufanyiwa vipimo katika Hospitali ya Vincent Pallotti jijini Cape Town, Afrika Kusini katikati ya wiki hii, imebainika kuwa Ngoma amekutwa na tatizo la kuchanika mtulinga wa mbele wa goti la mguu wa kulia (Anterior Cruciate Ligament).
    Mwankemwa aliyeongozana na Ngoma jijini humo amesema uchunguzi uliofanywa na madaktari hao kuangalia mtulinga huo (ligament) umebaini kwamba ameanza kupona na ataweza kurejea kwenye soka ya ushindani baada ya wiki tisa kutoka sasa.
    “Sasa matibabu yake ni nini, kwanza ni bahati yake kuwa yeye hatofanyiwa upasuaji atatakiwa kufanya mazoezi ya kawaida yasiyohusisha kulipa tabu goti lake (yatakayolishtua) kwa namna yoyote ile, katika wiki tatu hizi za kwanza kuanzia akiwa kwao Zimbabwe atatakiwa kufanya mazoezi madogo madogo.
    “Atakaporudi hapa baada ya wiki tatu kupita kuanzia sasa, Ngoma atakuwa Chamazi (Azam Complex) na atakuwa akienda kwenye kliniki ya London Health Centre ataendelea na ile programu na kuanza kukimbia kwa kasi na ataruhusiwa kurejea uwanjani kwa mechi za ushindani kuanzia Agosti 11 mwaka huu,” alisema Mwankemwa kwa msisitizo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YAKUBU AANZA KUJIFUA AZAM FC, NGOMA NJE WIKI TISA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top