• HABARI MPYA

  Thursday, June 07, 2018

  SOKA YA TANZANIA YAZIDI KUDIDIMIA, SASA NI WA 140 FIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  USHINDI wa mabao 2-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Machi 27 haujaisaidia Tanzania kuepuka maporomoko kwenye viwango vya soka vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa mwezi Aprili.
  Tanzania imeporomoka kwa nafasi tatu hadi ya 140 katika orodha ya Aprili – Mei iliyotolewa leo na FIFA, huku Ujerumani ikiendelea kuongoza duniani, ikifuatiwa na Brazil, Ubelgiji, Ureno, Argentina, Uswisi, Ufaransa, Poland, Chle na Hispania zikikamilisha 10 Bora.
  Kwa Afrika, Tunisia ndiyo inaongoza ikiwa nafasi ya 21 duniani, ikifuatiwa na Senegal 27, DRC 38, Morocco 41, Misri 45, Ghana 47, Nigeria 48, Cameroon 49, Mali 64 na Cape Verde 65 ikikamiklisha 10 Bora za Afrika.
  Mbwana Samatta akimiliki mpira mbele ya Aaron Tshibola wa DRC Machi 27
  Shiza Kichuya akijivuta kupiga shuti mbele ya Aaron Tshibola wa DRC Machi 27

  Tanzania inazidiwa na jirani zake wote wa Afrika Mashariki, Uganda ikikamata nafasi ya 82 na Kenya nafasi ya 112.
  Katika mchezo wa Machi 27 uliochezeshwa na marefa wa nyumbani, Elly Sasii aliyepuliza filimbi akisaidiwa na Ngazack Nduli na Mohamed Mkono, The Leopard ‘Chui wa DRC’ walikuwa wazuri kipindi cha kwanza na kukaribia mara kadhaa kufunga kama si ustadi wa safu ya ulinzi ya Stars chini ya mabeki Kelvin Yondan na Abdul Banda.
  Na baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, Taifa Stars wakabadilika kipindi cha pili na kuanza kung’ara uwanjani.
  Alianza Nahodha na mshambuliaji wa zamani wa Simba ya nyumbani na TP Mazembe ya DRC, Samatta kuifungia Taifa Stars bao la kwanza dakika ya 74 kwa kichwa akimalizia krosi ya Kichuya kutoka upande wa kulia.
  Kichuya akaifungia Tanzania bao la pili dakika ya 88 akimalizia pasi ya Samatta baada ya kazi nzuri ya winga wa Difaa Hassan El Jadidi ya Morocco, Simon Msuva.
  Tanzania iliingia kwenye mchezo wa leo ikitoka kufungwa 4-1 na Algeria mjini Algiers Machi 22 katika mchezo mwingine wa kirafiki na kwa ujumla huu ni ushindi wa kwanza kwa Taifa Stars ndani ya mechi 10, ikifungwa nne na sare tano.   
  Taifa Stars ilitoa sare mbili mfululizo na Rwanda kufuzu Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), 1-1 Julai 15 mjini Mwanza na 0-0 Julai 22 mjini Kigali, kabla ya kutoa sare nyingine za 1-1 mfululizo na Malawi mjini Dar es Salaam Oktoba 7 na Benin Novemba 12.
  Ikatoa sare ya 0-0 na Libya Desemba 3, ikafungwa 2-1 mara mbili, kwanza na Zanzibar Desemba 7, baadaye na Rwanda Desemba 9 na 1-0 na Kenya Desemba 11 kwenye michuano ya Challenge mjini Nairobi.
  Kwa Mei na Juni Taifa Stars haijacheza mechi maana yake hata orodha ya mwezi ujao itazidi kuiporomosha Tanzania kwenye renki za FIFA. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SOKA YA TANZANIA YAZIDI KUDIDIMIA, SASA NI WA 140 FIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top