• HABARI MPYA

    Friday, June 08, 2018

    SHAABAN IDDI CHILUNDA AWA MCHEZAJI BORA WA MWEZI WA MWISHO WA MSIMU LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa Azam FC ya Dar es Salaam, Shaaban Idd Chilunda amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Mei wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)Tanzania Bara.
    Chilunda alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Jacob Massawe wa Ndanda na Edward Shija wa Kagera Sugar katika uchambuzi uliofanywa wiki hii na kamati ya tuzo hizo.
    Chilunda aliisaidia Azam akifunga mabao 6 kwa mwezi huo, ambapo kati ya mabao hayo matatu ‘hat trick’ alifunga katika mchezo mmoja. 

    Shaaban Idd Chilunda amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Mei wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)Tanzania Bara

    Kwa mwezi huo Azam ilicheza michezo minne na kupata pointi tisa, baada ya kushinda michezo mitatu na kufungwa mmoja ikibaki katika nafasi yake ya pili na hakuwa na kadi yoyote.Kwa upande wa Shija aliisaidia Kagera Sugar kupata pointi 10, akifunga mabao matatu katika michezo minne iliyocheza timu yake, ikishinda mitatu na kutoka sare mmoja na kupanda kutoka nafasi ya 12 iliyokuwepo mwezi Aprili hadi ya tisa.
    Massawe alitoa mchango mkubwa katika kufanikisha timu yake kuepuka kushuka daraja ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matatu, akiisaidia kushinda mechi mbili kati ya nne walizocheza na hivyo kupanda katika msimamo wa ligi kutoka nafasi ya 15hadi ya 14 katika timu 16 zilizoshiriki ligi hiyo.Kutokana na ushindi huo, Chilunda atazawadiwa tuzo, kisimbuzi cha Azam na fedha taslimu sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini Vodacom.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SHAABAN IDDI CHILUNDA AWA MCHEZAJI BORA WA MWEZI WA MWISHO WA MSIMU LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top