• HABARI MPYA

  Wednesday, June 06, 2018

  MO DEWJI AANZA MAMBO SIMBA SC…AWAPIGA NA TUZO WACHEZAJI KIBAO KIKOSI CHA UBINGWA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MWANAHISA Mkuu mtarajiwa wa klabu ya Simba SC, Mohammed Gulam Dewji ameanzisha tuzo ambazo zitakuwa zikitolewa kwa wachezaji, viongozi na mashabiki wa klabu hiyo kila msimu, zikijulikana kwa jina la Mo Simba Awards.
  Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mo Dewji amesema kwamba mara ya kwanza tuzo hizi zitatolewa Jumatatu, Juni 11 katika hoteli ya Hyatt Regency – Kilimanjaro iliyopo mjini Dar es Salaam.
  Mo amesema kwamba tuzo hizo zitakuwa na vipengele 16, ambavyo ni Mchezaji Bora wa Mwaka, Goli Bora la Mwaka, Golikipa Bora wa Mwaka, Beki Bora wa Mwaka, Kiungo Bora wa Mwaka, Mshambuliaji Bora wa Mwaka, Shabiki Bora wa Mwaka na Tuzo ya Heshima.

  Mohamed 'Mo' Dewji ameshinda zabuni ya kununua asilimia 49 ya hisa katika mfumo mpya wa uendeshwaji

  Tuzo zingine ni Mchezaji Bora Mwanamke wa Mwaka, Mchezaji Bora Mdogo wa Mwaka, Tuzo ya Benchi la Ufundi, Kiongozi Bora wa Mwaka, Tuzo ya Wasimamizi wa Mchakato wa Mabadiliko, Mhamasishaji Bora wa Mwaka katika Mitandao ya Kijamii, Mhamasishaji Bora wa Mwaka na Tawi Bora la Mwaka.
  Washindi wa tuzo hizo watatokana na kura ambazo zitapigwa na mashabiki kupitia mitandao ya kijamii na tovuti ya mosimbaawards.co.tz na kamati maalumu ya tuzo ambayo itahusisha wadau mbalimbali wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.
  Dewji amesema ameanzisha tuzo hizo kwa lengo la kutambua mchango wa wachezaji, viongozi na mashabiki ambao juhudi zao zimeiwezesha Simba SC kupata mafanikio iliyonayo sasa.
  Dewji amesema tuzo hizo ni sehemu ya mikakati yake ya kuifanya klabu ya Simba kuwa timu kubwa barani Afrika, ambayo itakuwa na uwezo wa kifedha ambao utaiwezesha kuwa na wachezaji na benchi la ufundi bora ambalo litaiwezesha kushinda mataji makubwa.
  “Simba ni timu kubwa inastahili kuwa na tuzo zake ambazo zitakuwa zinatolewa kwa kutambua mchango wa wenzetu ambao umetuwezesha kupata mafanikio haya ikiwepo kushinda taji la Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Ni jambo ambalo litawatia moyo kuendelea kujituma lakini hata kwa ambao watakosa itawatia hamasa na hivyo kuongeza juhudi,” amesema Dewji.
  Aidha, Mo amesema kwamba tafrija hiyo ya utoaji wa tuzo hizo itaonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV.
  Simba SC imemaliza vizuri msimu, ikitwaa mataji mawili, kwanza Ngao ya Jamii na baadaye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuelekea zama mpya za kumilikiwa na Mo Dewji, ameshinda zabuni ya kununua asilimia 49 ya hisa katika mfumo mpya wa uendeshwaji. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MO DEWJI AANZA MAMBO SIMBA SC…AWAPIGA NA TUZO WACHEZAJI KIBAO KIKOSI CHA UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top