• HABARI MPYA

    Wednesday, June 13, 2018

    REAL MADRID YAMPONZA LOPETEGUI ATIMULIWA HISPANIA

    KOCHA Julen Lopetegui amefukuzwa timu ya taifa ya Hispania kuelekea Kombe la Dunia baada ya wakuu wa Chama cha Soka (FA) kukerwa na kuteuliwa kwake kuwa kocha mkuu wa Real Madrid.
    Mkuu wa FA ya Hispania, Luis Rubiales leo amefanya mkutano na Waandishi wa Habari na kuelezea namna alivyokerwa na tangazo lake la kuhamia Real Madrid.
    Pamoja na wachezaji wa Hispania kumsihi Rubiales kumuacha kazini Lopetegui, lakini imeamuliwa aondoke mara moja. 
    Fernando Hierro, mchezaji wa zamani wa Real Madrid amethibitishwa kuwa mbadala wa Lopetegui wakati huu wa mashindano ya Kombe la Dunia, Hispania wakifungua dimba na Ureno usiku wa Ijumaa.
    Julen Lopetegui amefukuzwa timu ya taifa ya Hispania baada ya kuteuliwa kwake kuwa kocha mkuu wa Real Madrid 

    Kipa huyo wa zamani wa kimataifa wa Hispania, Julen Lopetegui jana alitambulishwa kuwa kocha mpya wa Real Madrid wiki kadhaa baada ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kufundisha timu ya taifa
    Lopetegui amesaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kufundisha Hispania hadi Mei 22 mwaka 2020, lakini Real Madrid wamemnyakua na amekubali kujikunga na vigogo hao wa Madrid baada ya fainali za Kombe la Dunia. 
    Kocha huyo mwenye umri wa miaka 51, enzi zake aliichezea Barcelona kwa miaka mitatu, lakini sasa atafanya kazi kwa wapinzani. 
    Real Madrid imesema kwamba Julen Lopetegui atakuwa kocha wao wa kikosi cha kwanza kwa misimu mitatu ijayo, akichukua nafasi ya Mfaransa, Zinadine Zidane aliyeondoka mwezi uliopita baada ya kuipa klabu taji la tatu mfululizo la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
    Na kutua kwake kunazima tetesi zilizokuwa zimezagaa kwamba Arsene Wenger, Antonio Conte na Guti walikuwa wanapewa nafasi ya kumrithi Zidane.    
    Lopetegui, ambaye amekuwa kocha wa timu ya taifa ya Hispania kwa miaka miwili iliyopita, amekubali mkataba wa miaka mitatu kufanya kazi Bernabeu.
    Inamaanisha Lopetegui, ambaye awali alifundisha timu za Porto, Rayo Vallecano na Real Madrid B kwa mwaka mmoja, atawafundisha wapinzani wakubwa wa Barcelona nchini Hispania wiki chache zijazo. 
    Lopetegui alionekana akizungumza na nyota wa Barcelona, Gerard Pique katika kambi ya timu ya taifa huko Krasnodar kabla ya Real Madrid kutangaza uteuzi wake. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: REAL MADRID YAMPONZA LOPETEGUI ATIMULIWA HISPANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top