• HABARI MPYA

  Tuesday, June 12, 2018

  KIPA WA ZAMANI WA BARCELONA AWA KOCHA MPYA REAL MADRID

  KIPA wa zamani wa kimataifa wa Hispania, Julen Lopetegui ametambulishwa kuwa kocha mpya wa Real Madrid wiki kadhaa baada ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kufundisha timu ya taifa
  Lopetegui amesaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kufundisha Hispania hadi Mei 22 mwaka 2020, lakini Real Madrid wamemnyakua na amekubali kujikunga na vigogo hao wa Madrid baada ya fainali za Kombe la Dunia. 
  Kocha huyo mwenye umri wa miaka 51, enzi zake aliichezea Barcelona kwa miaka mitatu, lakini sasa atafanya kazi kwa wapinzani. 

  Julen Lopetegui ametambulishwa kuwa kocha mpya wa Real Madrid akimrithi Mfaransa Zinadine Zidane 
  Real Madrid imesema katika taarifa yake rasmi: "Julen Lopetegui atakuwa kocha wa Real Madrid baada ya sherehe za Kombe la Dunia 2018,".
  Real Madrid imesema kwamba Julen Lopetegui atakuwa kocha wao wa kikosi cha kwanza kwa misimu mitatu ijayo, akichukua nafasi ya Mfaransa, Zinadine Zidane aliyeondoka mwezi uliopita baada ya kuipa klabu taji la tatu mfululizo la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
  Na kutua kwake kunazima tetesi zilizokuwa zimezagaa kwamba Arsene Wenger, Antonio Conte na Guti walikuwa wanapewa nafasi ya kumrithi Zidane.    
  Lopetegui, ambaye amekuwa kocha wa timu ya taifa ya Hispania kwa miaka miwili iliyopita, amekubali mkataba wa miaka mitatu kufanya kazi Bernabeu.
  Inamaanisha Lopetegui, ambaye awali alifundisha timu za Porto, Rayo Vallecano na Real Madrid B kwa mwaka mmoja, atawafundisha wapinzani wakubwa wa Barcelona nchini Hispania wiki chache zijazo. 
  Lopetegui alionekana akizungumza na nyota wa Barcelona, Gerard Pique katika kambi ya timu ya taifa huko Krasnodar kabla ya Real Madrid kutangaza uteuzi wake. 
  Sergio Ramos, Dani Carvajal, Nacho, Lucas Vazquez, Marco Asensio na Isco wote hao kwa sasa wapo kwenye kikosi cha wachezaji 23 wa timu ya taifa chini ya Lopetegu. 
  Lopetegui ambaye alikaribia kufundisha Wolves kabla ya kujiunga na Hispania mwaka 2016, atapata fursa ya kumuona nyota mkubwa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo wakati wa mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia Ijumaa jioni. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIPA WA ZAMANI WA BARCELONA AWA KOCHA MPYA REAL MADRID Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top