• HABARI MPYA

  Thursday, April 13, 2023

  SOKA YA WANAWAKE MAMBO SAFI, WANAUME…


  TANZANIA imetoa bingwa wa soka wa shule za Sekondari barani Afrika kwa wasichana kufuatia shule ya Fountain Gate ya Dodoma kutwaa taji hilo wiki iliyopita Jijini Durban, Afrika Kusini.
  Ni matokeo ambayo yamemfurahisha hadi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye ameipongeza Fountain Gate kwa kutwaa ubingwa huo.
  "Nawapongeza Timu ya Wasichana ya Mpira wa Miguu ya Sekondari ya Fountain Gates Dodoma, kwa kutwaa ubingwa kwenye Mashindano ya Soka kwa Shule za Sekondari ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF African Schools Continental Champions), upande wa wasichana," alisema Rais Samia.
  Rais Dk. Samia alisema ushindi huo unakwenda sambamba na nia ya Serikali yake kuendelea kuboresha mtaala wa elimu nchini katika kukuza si tu elimu ya darasani, bali na vipaji pia, ili kupata wahitimu wengi zaidi wenye uwezo wa kutumia maeneo hayo mawili muhimu kuleta maendeleo.
  Aprili 8, mwaka huu Fountain Gate ilitwaa ubingwa wa michuano ya shule za sekondari Afrika kwa wasichana baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Ecole Omar IBN Khatab ya Morocco Uwanja wa King Zwelithini Jijini Durban, Afrika Kusini.
  Katika michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), mabao ya Fountain Gate yalifungwa na Winfrida Gerald Hubert mawili na Irene Chitanda moja na huo ulikuwa mchezo wa pili siku hiyo baada awali kuitandika SCG De Mfilou ya Kongo mabao 4-0 katika Nusu Fainali.
  Fountain Gate pia imetoa Mchezaji Bora wa Mashindano, Wilifrida Gerald Hubert ambaye pia ameibuka Mfungaji Bora kwa mabao yake 11, na Kipa Bora, Allic Neckema.
  Kwa kutwaa ubingwa huo, Fountain Fate ilizawadiwa dola za Kimarekani 300,000, kiasi ambacho pia amepewa bingwa wa upande wa wavulana, huku washindi wa pili wakiondoka na dola 200,000 na wa tatu dola 150,000.
  Mashindano hayo ya shule ya za sekondari Afrika hayakuwa kwa wasichana pekee, yalihusu wavulana pia ambako bingwa wake ni shule ya Scolaire Ben Sekou Sylla ya Guinea ambayo iliwafunga wenyeji, Clapham High School kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya 1-1 hapo hapo Durban.
  Salima Secondary School ya Malawi ilifanikiwa kushika nafasi ya tatu kwa wavulana baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya CEG Sainte Rita ya Benin.
  Mchezaji Bora ni Kagiso Maloka wa Clapham High School kwa wavulana na mabingwa, CS Ben Sekou Sylla wametoa Kipa Bora Ibrahima Camara wa na mfungaji Bora Mohamed Sacko aliyefunga mabao sita akimzidi moja mchezaji mwenzake wa timu hiyo ya Guinea, Amara Keita.
  Hapana shaka Watanzania wangetamani kuona hata bingwa wa wavulana wa michuano hiyo anatoka nchini kwao, kwa sababu huo ni msingi mzuri wa kuwa na timu bora baadaye.
  Mambo yanakwenda vizuri katika soka ya wanawake kuliko kwenye soka ya wanaume – kwani inakumbukwa ni Oktoba mwaka jana tu timu ya mabinti chini ya umri wa miaka 17 ilikuwa kati ya wawakilishi watatu wa Afrika kwenye Fainali za Kombe la Dunia nchini India, wengine Morocco na Nigeria.
  Kwenye soka ya wasichana hakuna uwekezaji mkubwa zaidi ya uliopo kwenye mpira wa miguu wa wavulana kwa ujumla, lakini matokeo yamekuwa ya kuvutia zaidi upande mmoja.
  Ni jukumu la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Kamati yake ya Soka ya Vijana na Kurugenzi ya Ufundi kufanya tathmini ya kina ili kujua kiini cha kuzorota kwa soka ya wavulana siku za karibuni.
  Wakati ambao Ligi zetu zote Kuu za wanaume na wanawake zimesheheni wanasoka wa kigeni, tunahitaji msingi imara wa soka ya vijana chini ili kuzalisha vipaji zaidi ya kuja kushindana na wageni.
  Zaidi ni kuzalisha wachezaji wazuri kwa ajili ya timu zetu za taifa baadaye, kwa maana hao wanaozifanya Simba na Yanga zitambe kwenye michuano ya klabu barani Afrika – inapowadia kalenda ya Kimataifa wanakwenda kuzitumikia nchi zao na sisi tunabaki na wazawa wetu.
  Hivyo, wakati tunatoa pongezi kwa Fountain Gate kutwaa ubingwa wa shule za sekondari kwa wasichana Afrika, tutazame pia na namna ambavyo tunaweza kuifanya nchi yetu ing’are na kwenye soka ya wavulana Kimataifa ili kujenga msingi mzuri wa timu zetu za taifa baadaye. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SOKA YA WANAWAKE MAMBO SAFI, WANAUME… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top