• HABARI MPYA

    Wednesday, April 26, 2023

    MAWAZIRI WA MICHEZO WA NCHI 14 KUKUTANA ARUSHA


    TANZANIA itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa nchi 14 Wanachama wa Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika, Kanda ya Nne wa Mawaziri na Wakurugenzi wa Michezo utakaofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 2 hadi 4 Mei, 2023. 
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Arusha Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu amesema mkutano huo unafanyika nchini kufuatia maombi ya Tanzania kukubaliwa na Baraza hilo ambalo liko chini ya Umoja wa Afrika (AU) na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, (Mb) atakuwa mgeni rasmi.
    “Tanzania tumepewa heshima kubwa ya kuandaa mkutano huu muhimu kutokana na kukua kwa Diplomasia ya michezo ya nchi yetu Kimataifa, Timu zetu sasa zinafanya vizuri katika michezo na mashindano ya Kimataifa pia ni fursa muhimu kwa nchi yetu kuendelea kujitangaza Kimataifa na pia kuonesha jinsi gani Tanzania inaweza kuandaa mikutano mikubwa ya aina hii. Amesisitiza Saidi Yakubu.
    Ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa msukumo mkubwa katika Sekta ya Michezo kuhakikisha Tanzania inaendelea kufanya vizuri kwenye sekta ya Michezo akibainisha kuwa viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri na Wakurugenzi wa Michezo kutoka nchi 14, Makatibu Wakuu, Viongozi wa Mabaraza ya Michezo, Mashirikisho na Vyama vya Michezo watahudhuria mkutano huo utakaotoa fursa kwa Tanzania kupata nafasi nzuri zaidi ya kuwa mwenyeji wa Makao Makuu ya kudumu ya Sekretarieti ya Baraza la Michezo Umoja wa Afrika, Kanda ya Nne jambo litakaloongeza ajira na fursa za michezo kwa Watanzania.
    Nchi 14 wanachama wa Baraza hilo ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia, Sudan, Sudani Kusini, Eritrea, Somalia, Djibouti, Maritious, Madagascar, Comoro na Seychelles zitashiriki mkutano huo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAWAZIRI WA MICHEZO WA NCHI 14 KUKUTANA ARUSHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top