• HABARI MPYA

    Wednesday, April 19, 2023

    INONGA NA MAYELE, LADHA MPYA MECHI YA WATANI WA JADI

     

    LINAPOWADIA pambano la watani wa jadi katika soka ya Tanzania hivi sasa gumzo kubwa ni wachezaji wawili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), beki Henock Inonga Baka ‘Varane’ Simba na mshambuliaji Fiston Kalala Mayele wa Yanga.
    Upinzani wa uwanjani wa wawili hao hakika unakumbushia upinzani wa wachezaji wengine kadhaa kwenye mechi za Simba na Yanga tangu miaka ya 1960.
    Miongoni mwa wachezaji waliojipatia umaarufu kwenye mechi za watani wa jadi miaka ya 1980 kwa upinzani wao wa uwanjani ni beki wa Yanga, Athumani Juma ‘Chama’ au Jogoo dhidi ya mshambuliaji wa Simba, Zamoyoni Mogela.
    Hii imezaa hadi msemo maarufu wa ‘Chama na Mogella’, ikimaanisha watu wanaogandana au kuwa pamoja mara nyingi.
    Lakini baadaye miaka ya 1990 ushindani baina ya beki wa Simba, Kasongo Athumani na mshambuliaji wa Yanga, Edibily Lunyamila nao pia ulikuwa gumzo.
    Miaka ya 2000 ilijitokeza burudani nyingine baina ya mshambuliaji wa Simba, Mussa Hassan Mgosi dhidi ya beki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
    Lakini kwa sasa kwenye mechi za watani, gumzo kubwa ni baina ya wachezaji hao wawili kutoka Kongo, kutokana na namna wanavyopaniana na mbwembwe zao za uwanjani baina yao.
    Wawili hao ambao wote wana miaka 28 kwa sasa, walisajiliwa msimu mmoja Tanzania 2021-2022, Mayele ambaye Juni 24, akitokea AS Vita na Inonga akitokea DC Motema Pembe, zote za Kinshasa. 
    Mechi ya kwanza ya watani baada ya wawili hao kusajiliwa nchini ilikuwa ni ya Ngao ya Jamii Septemba 25, 2021 na kocha wa Simba, Mfaransa Didier Gomes Da Rosa hakumpa hata jezi Inonga akiwaanzisha Mkenya, Joash Onyango na Muivory Coast, Serge Wawa katika beki ya kati.
    Upande wa Yanga, Mtunisia Nasredine Nabi alimuanzisha Mayele na ndiye aliyekwenda kufunga bao pekee dakika ya 11, Yanga ikibeba taji la kwanza kati ya matatu iliyokusanya mwishoni mwa msimu, mengine ubingwa wa Ligi Kuu na Azam Sports Federation Cup.
    Oktoba 26 mwaka 2021, Gomes akafukuzwa Simba baada ya timu kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia kuchapwa 3-1 nyumbani na Jwaneng Galaxy ya Botswana na kocha mpya, Mspaniola Pablo Franco Martin akampanga Inonga kwa mara ya kwanza kwenye mechi ya watani Desemba 11, mwaka 2021.
    Inonga alimdhibiti vilivyo Mayele na mchezo huo ukamalizika kwa suluhu, huku beki huyo wa Simba akimsindikiza kwa mbwembwe mshambuliaji wa Yanga nje ya Uwanja, akimaanisha yeye ndiye kiboko yake.
    Hali ikawa hivyo tena kwenye mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Aprili 30, Inonga akimdhibiti ipasavyo Mayele nakumaliza mchezo bila kufunga, timu hizo zikitoka bila bila tena.
    Mei 28, mwaka 2022 timu hizo zilikutana tena katika Nusu Fainali ya Azam Sports Federation Cup na pamoja na Inonga kumzuia Mayele kufunga, lakini Yanga ilishinda 1-0 kwa bao pekee la kiungo Feisal Salum Abdallah dakika ya 25 Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza. 
    Agosti 13, mwaka 2022 katika mchezo wa Ngao ya Jamii winga Msenegal, Pape Ousmane Sakho alianza kuifungia Simba dakika ya 16, kabla ya Mayele kuisawazishia Yanga dakika ya 50 na kufunga bao la pili dakika ya 81 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
    Baada ya mechi Yanga wakishangilia ushindi wa Ngao, Mayele alikwenda kumbeza Inonga wakati anaondoka uwanjani akilipa kisasi cha yeye kufanyiwa hivyo na Mkongo mwenzake huyo.
    Tangu hapo picha ya nani zaidi baina yao imekuwa kubwa na upinzani wao unatarajiwa kuwa sehemu kubwa ya buruani ya mechi ya watani.
    Ikumbukwe mechi ya kwanza ya msimu huu ya watani ilimalizika kwa sare ya 1-1, Oktoba 23, mwaka 2022, Mghana Augustine Okrah akiitanguliza Simba dakika ya 15, kabla ya Mburkinabe, Stephane Aziz Ki kuisawazishia Yanga dakika ya 45.
    Inonga Baka ‘Varane’ wa Kongo akawa na siku nzuri Aprili 16, mwaka 2024,kwani licha ya kumdhibiti Mayele asifunge bao kwenye mechi ya marudiano ya Ligi Kuu, lakini akafunga bao la mapema dakika ya pili la Simba kabla ya Kibu Dennis Prosper kufunga la pili dakika ya 32 katika ushindi wa 2-0 Uwanja wa Benjamin Mkapa. 
    Ilikuwa inafurahisha namna ambavyo Inonga alikuwa akimbana Mayele asiweze kufurukuta na baada ya mchezo akaenda kumtafuta kumbeza kama ilivyo ada yao.
    Inatamanisha kuona nini kitaendelea baina ya wawili hao kwenye mchezo ujao wa watani. Inonga na Mayele, ladha mpya ya pambano la watani wa jadi nchini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: INONGA NA MAYELE, LADHA MPYA MECHI YA WATANI WA JADI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top