• HABARI MPYA

  Wednesday, April 26, 2023

  NA IKAWE WIKIENDI YA KIHISTORIA KATIKA SOKA YA TANZANIA


  WIKIENDI hii Tanzania itawania kupeleka timu mbili kwenye Nusu Fainali za michuano ya klabu Afrika kwa mara ya kwanza kihistora, wakati Simba na Yanga zitakapoteremka dimbani kuwania nafasi hiyo.
  Simba SC watakuwa Uwanja wa Mohamed V Jijini Casablanca nchini Morocco kuanzia Saa 4:00 usiku kumenyana na wenyeji, Wydad Club Athletic katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Siku hiyo Simba itakuwa inahitaji sare tu ili kwenda Nusu Fainali baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya mabingwa hao watetezi Jumamosi, bao pekee la mshambuliaji Mkongo, Jean Othos Baleke dakika ya 30 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Wakati Wydad ina mataji matatu ya CAF Champions League (1992, 2017 na 2021–22), mafaniko makubwa kwa Simba kwenye michuano hiyo ni kufika Nusu Fainali mwaka 1974 ilipoitoa Hearst Of Oak ya Ghana kwa mabao 2-1 kabla ya kutolewa na Ghazl El Mahalla yenye maskani yake mji wa El Mahalla El Kubra kwa penalti 3-0 kufuatia sare ya jumla ya 1-1.
  Upande wa Yanga wao watakuwa nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam Jumapili kumenyana na Rivers United ya Nigeria katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
  Yanga SC nao hata kwa sare watakwenda Nusu Fainali baada ya ushindi wa 2-0 kwenye mchezo wa kwanza Jumapili Uwanja wa Godswill Akpabio International mjini Uyo, mabao yote ya mshambuliaji Mkongo, Fiston Kalala Mayele dakika ya 73 na 81.
  Mafanikio makubwa ya Yanga katika michuano ya Afrika ni kufika Robo Fainali tu mara nne, mara tatu katika Ligi ya Mabingwa 1969, 1970 na 1998 na mara moja katika Kombe la Washindi 1995.
  Kwa Rivers United iliyoanzishwa mwaka 2016, ukiwa ni muungano wa klabu mbili za jimbo la Port Harcourt, Dolphins FC na Sharks FC – hatua waliofika sasa ndio kubwa zaidi kwao, kwani awali 2017 waliishia raundi ya kwanza, 2022 Raundi ya pili Ligi ya Mabingwa, 2017 hatua ya makundi kombe la shirikisho na 2020-21 na 2021-22 zote hatua ya mchujo kuwania kuingia makundi.
  Kabla ya Muungano wao, Sharks FC haikuwa na maajabu kwenye soka ya Afrika, lakini Dolphins FC walifika Robo Fainali Ligi ya Mabingwa mwaka 1998 na kwenye Kombe la Shirikisho mwaka 2005 walifika Fainali wakafungwa na FAR Rabat 3-0 Morocco baada ya wao kushinda 1-0 Port Harcourt.
  Kuelekea mechi za marudiano wikiendi hii, matumaini ni makubwa zaidi kwa Yanga baada ya ushindi wa ugenini, huku Simba wakionekana kwenda kwa tahadhari kubwa Morocco kwa sababu hawaamini silaha ya ushindi wa 1-0 nyumbani.
  Kuna wenye kujipa moyo kwamba Simba inaweza kurudia ilichokifanya mwaka 2003 kuwatoa Zamalek wakiwa mabingwa wa Afrika na kuingia Robo Fainali. 
  Ilikuwa kama dhidi ya mabingwa wa sasa, Wydad; Simba iliichapa Zamalek 1-0 Jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 1-0 Cairo na kwenye mikwaju ya penalti Wekundu wa Msimbazi wakashinda 3-2.
  Pongezi kwa timu zetu zote kwa matokeo ya awali – hususan Yanga walioshinda ugenini, kwani inafahamika ushindi wa ugenini si jambo jepesi hata ukicheza na timu dhaifu, kwani ni msimu huu katika hatua za awali za Ligi ya Mabingwa Rivers waliifunga Wydad 2-1.
  Simba wanaweza kurudia walichokifanya mwaka 2003 kwa Zamalek kama watakwenda na mpango kazi mzuri kwenye mechi ya Ijumaa na kuwadhibiti vizuri Wydad, jambo ambalo linawezekana chini ya kocha Mbrazil, Robert Oliveira ‘Robertinho’.
  Kwa Yanga wanapaswa kujua tabia za Wanigeria ni kutokata tamaa na wamekwishatudhihirishia hapa Tanzania mara kadhaa kwa kupata matokeo magumu kwao na kuja kushinda kwenye ardhi yetu – hivyo wana Jangwani wajipange kupambana hapa washinde pia ili waende Nusu Fainali.
  Kila la heri Simba na Yanga. Nusu Fainali ipo uani kwenu. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NA IKAWE WIKIENDI YA KIHISTORIA KATIKA SOKA YA TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top