• HABARI MPYA

  Sunday, April 30, 2023

  ROBERTINHO AELEKEZA NGUVU ZAKE UBINGWA WA LIGI KUU YA TANZANIA BARA


  KOCHA Mbrazil wa Simba, Robert Oliveira ‘Robertinho’ amesema kwamba amehamishia nguvu zake kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Mbio za Simba SC katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara nyingine ziliishia hatua ya Robo Fainali baada ya kutolewa na mabingwa watetezi, Wydad Club Athletic Ijumaa kwa penalti 4-3  Uwanja wa Mohamed V Jijini Casablanca, Morocco.
  Dakika 90 zilimalizika kwa Wydad AC kushinda 1-0, bao pekee la mshambuliaji Msenegal, Bouly Junior Sambou dakika ya 24 kwa kichwa na kufanya sare ya jumla ya 1-1 kufuatia Simba kushinda 1-0 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita Dar es Salaam, bao la mshambuliaji Mkongo Jean Othos Baleke dakika ya 31.
  Kuelekea mechi nne za mwisho za Ligi Kuu, Simba inashika nafasi ya pili kwa pointi zake 63, ikizidiwa pointi tano na mabingwa watetezi, Yanga SC baada ya wote kucheza mechi 26.
  Wekundu hao wa Msimbazi wana mechi moja tu ugenini dhidi ya Namungo FC Jumatano Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi lakini tatu nyingine dhidi ya Ruvu Shooting, Polisi Tanzania na Coastal Union zitafuatia Dar es Salaam.
  Lakini pia Simba ipo Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) na Jumamosi watamenyana na Azam FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, hayo yakiwa mataji pekee mawili yaliyobaki wanayowania.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ROBERTINHO AELEKEZA NGUVU ZAKE UBINGWA WA LIGI KUU YA TANZANIA BARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top