• HABARI MPYA

  Jumatano, Septemba 04, 2019

  TAIFA STARS YALAZIMISHA SARE YA 1-1 NA BURUNDI LEO BUJUMBURA KUFUZU KOMBE LA DUNIA

  Na Mahmoud Zubeiry, BUJUMBURA
  TANZANIA imejiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye mbio za kuwania tiketi ya Kombe la Dunia 2022 Qatar baada ya kulazimisha sare ya 1-1 na wenyeji, Burundi leo Uwanja wa Intwari mjini Bujumbura.
  Kwa matokeo hayo, Taifa Stars itahitaji hata sare ya bila mabao kwenye mchezo wa marudiano Jumapili Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam ili iweze kusonga mbele. 
  Baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, Taifa Stars inayofundishwa na kocha Mrundi, Etienne Ndayiragijje wakitawala vizuri mchezo kabla ya wenyeji kufunguka mwishoni mwa kipindi hicho, mambo yalibadilika kipindi cha pili.
  Nyota wa Tanzania, Simon Msuva akitafuta maarifa ya kuwatoka wachezaji wa Burundi leo Bujumbura

  Mshambuliaji wa Al Taawon ya Saudi Arabia, Cedric Amissi akawatanguliza wenyeji kwa bao zuri dakika ya 78, akimalizia pasi ya wa jina lake, Amissi Mohammed wa NAC Breda ya Uholanzi kutoka upande wa kushoto, ambaye alifanikiwa kuwatoka kiungo wa ENNPI ya Ethioppia, Himid Mao na beki wa Simba SC ya nyumbani, Ramadhani Haruna Shamte.
  Kiungo mshambuliaji wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Simon Happugod Msuva akaisawazisjhia Tanzania dakika ya 84 akimalizia mpira uliorudi baada ya kumgonga beki wa Burundi, Frederic Nsabiyumva kufuatia pigo la Mao. 
  Na sifa zimuendee pia Nahodha na mshambuliaji wa KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Ally Samatta alimsumbua beki huyo hadi akashindwa kuokoa na mpira ukamgonga na kumtoka. 
  Na pongezi pia kwa safu ya ulinzi ya Tanzania ikiongozwa na wakongwe, kipa Juma Kaseja Juma na mabeki Erasto Edward Nyoni na Kelvin Patrick Yondan kwa kufanikiwa kumdhibiti mshambuliaji hatari wa Burundi, Saido Berahino anayechezea Zulte-Waregem ya Ubelgiji asilete madhara leo.
  Mshindi wa jumla katika mchezo wa Jumapili ataingia kwenye moja ya makundi 10 kuwania kwenda hatua ya mwisho ya mchujo wa mbio za Qatar 2022.
  Timu zitakazoongoza makundi katika hatua hiyo zitamenyana baina na washindi watano ndio watakaoiwakilisha Afrika kwenye Kombe la Dunia lijalo, Qatar.
  Kikosi cha Burundi kilikuwa; Jonathan Nahimana, Ramazani Diamant, Joel Bacanamwo, Frederic Nsabiyumva, David Nshimimana, Pierre Kwizera/Duhayindavi Gael dk9, Gael Bigirimana, Cedric Amissi, Biemvenu Kanakimana/Amissi Mohamed dk61, Bon Fils Caleb Bimenyimana/Abdulrazak Fiston k41 na Sado Berahino. 
  Tanzania; Juma Kaseja, Ramadhani Shamte, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Kelvin Yondan, Jonas Mkude, Himid Mao/Farid Mussa dk86, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Frank Domayo dk65, Mbwana Ally Samatta, Simon Msuva na Hassan Dilunga/Iddi Nado dk55.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TAIFA STARS YALAZIMISHA SARE YA 1-1 NA BURUNDI LEO BUJUMBURA KUFUZU KOMBE LA DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top