• HABARI MPYA

  Jumatatu, Septemba 16, 2019

  MANULA NA KAPOMBE WAACHWA TENA TAIFA STARS KIKOSI CHA KUIVAA SUDAN JUMAPILI DAR

  Na Saada Salim, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars Etienne Ndayiragije ameita wachezaji 25 kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) mwakani nchini Cameroom dhidi ya Sudan utakaofanyika Jumapili wiki hii mjini Dar es Salaam.
  Lakini katika kikosi hicho, Ndayiragijje ameendelea kutomjumuisha kipa bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na kipa wa kwanza wa muda mrefu wa Taifa Stars, Aishi Salum Manula japo yuko fiti kwa sasa na ameidakia klabu yake, Simba SC mechi zote tatu zilizopita.
  Awali kabisa kwenye mchezo wa Raundi ya kwanza ya kufuzu CHAN dhidi ya Kenya, Ndayiragijje alimuacha Manula kwa sababu za kuwa majeruhi, lakini kipa huyo alirejea mwanzoni tu mwa msimu, Agosti na ameendelea kudaka hadi Ijumaa iliyopita, SImba ikishinda 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar. 

  Aidha, Ndayiragijje aliyeisaidia Tanzania kuifuzu hatua ya makundi ya kuwania tiketi ya fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar baada ya kuitoa Burundi kwa penalti 3-0 kufuatia sare ya jumla ya 2-2, pia amemuacha beki mkongwe wa kulia Shomari Salum Kapombe na kuwachukua Haruna Ramadhani Shamte, wote wa Simba na Boniphace Maganga wa KMC.
  Kwa ujumla kikosi cha Taifa Stars kilichotajwa leo na Mrundi huyo kinaundwa na Makipa; Juma Kaseja (KMC), Metacha Mnata (Yanga SC) na Said Kipao (Kagera Sugar).
  Mabeki; Haruna Shamte (Simba), Boniphace Maganga (KMC), Gardiel Michael (Simba SC), Mohammed Hussein (Simba), Kelvin Yondan, Erasto Nyoni (Simba), Iddy Mobi (Polisi Tanzania), Bakarei Mwamnyeto (Coastal Union).
  Viungo; Jonas Mkude (Simba SC), Baraka Majogoro (Polisi Tanzania), Mohammed Issa ‘Banka’ (Yanga SC), Mudathir Yahya (Azam FC), Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Azam FC), Frank Domayo (Azam FC), Muzamil Yassin (Simba SC), Abdulaziz Makame (Yanga SC), Hassan Dilunga (Simba SC) na Feisal Salum.  
  Washambuliaji; Iddi Suleiman ‘Nado’ (Azam FC), Miraj Athumani ‘Madenge’ (Simba SC), Shaaban Iddi Chilunda (Azam FC) na Ayoub Lyanga (Coastal Union). 
  Taifa Stars watakuwa wenyeji wa Sudan Septemba 22 mjini Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana Oktoba  18 mjini Kampala nchini Uganda. Sudan wamechagua kurudiana na Stars Uganda kwa sababu ya machafuko yanayoendelea nchini kwao.
  Manula amekuwa kipa wa kwanza Tanzania tangu mwaka 2017 akiiwezesha Taifa Stars kufuzu tena Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zilizofanyika nchini Misri Juni mwaka huu, ikiwa ni mara ya pili kihistoria kwa nchi baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria. 
  Na kwa kipindi chote hicho pia Manula aliyeibukia Azam FC mwaka 2013 kabla ya kuhamia Azam FC miaka miwili iliyopita amekuwaa akitwaa mfululizo tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu, wakati Kapombe inaaminika ndiye beki bora zaidi wa kulia nchini kwa sasa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MANULA NA KAPOMBE WAACHWA TENA TAIFA STARS KIKOSI CHA KUIVAA SUDAN JUMAPILI DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top