• HABARI MPYA

  Jumatano, Septemba 18, 2019

  KIUNGO WA ZAMANI WA SIMBA SC NA AZAM FC IBRAHIM JEBA AFARIKI DUNIA KWAO ZANZIBAR

  Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
  KIUNGO wa zamani wa klabu za Azam FC, Simba SC za Dar es Salaam na Mtibwa Sugar ya Morogoro, Ibrahim Rajab Juma ‘Jeba’ amefariki dunia jioni ya leo nyumbani kwao, kisiwani Zanzibar akiwa ana umri wa miaka 26.
  Jeba aliyewahi pia kuchezea timu za taifa kuanzia za vijana nchini kuanzia chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, U20, Ngorongoro Heroes, U23 na ya wakubwa, Taifa Stars umauti umemkuta katika hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar alipopelekwa kwa matibabu ya moyo.
  Juni mwaka 2012 Jeba alisajiliwa na Simba, hata hivyo pamoja na kujiunga nayo kwa mazoezi lakini hakuweza kuichezea baada ya kuwekewa ngumu na Azam FC iliyokuwa na mkataba naye wa miaka miwili.
  Buriani Ibrahim Rajab Juma 'Jeba' (kushoto). Hapa ni wakati akiwa Mtibwa Sugar anampita beki wa Simba SC, Mohammed Hussein 'Tshabalala' Uwanja wa Amaan, Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka 2016 siku ambayo aliifungia bao pekee la ushindi timu yake ikitinga fainali 
  Ibrahim Jeba (kushoto) akiwa na wachezaji wenzake wa Azam FC wakati huo, John Bocco na Himid Mao

  Lakini baadaye Azam FC ikasema Jeba hatakiwi kuendelea kucheza soka ya ushindani, kwani vipimo vimeonyesha ana matatizo ya moyo. Hata hivyo Jeba aliendelea na soka ya ushindani na mwaka 2017 alijiunga na Mtibwa Sugar, klabu yake ya mwisho kucheze Bara.
  Jeba aliyezaliwa Agosti 14, mwaka 1993, kipaji chake cha soka kilianza kuonekana wakati anapata elimu yake ya Msingi katika shule ya Mwanakwerekwe huko Zanzibar, wakati ambao pia alichezea timu za Simba Kids na Lebanon za huko.
  Mwaka 2007 alijiunga na klabu ya Ras El Khalima iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza la Zanzibar, kabla ya kuhamia Ochu Boys ya Daraja la Pili, ambazo zilimfanya mwaka 2010 achaguliwe Kombaini ya Mkoa wa Mjini Magharibi kwa ajili ya michuano ya Copa Coca Cola.
  Na ni kwenye michuano hiyo ndipo Azam ilipomuona na kumjumuisha katika kikosi chao cha vijana wenye umri chini ya miaka 20 kuanza rasmi safari yake ya kisoka.
  Msimu huu Jeba alikuwa amekwishaanza mazoezi na timu yake ya Chuoni kwa ajili ya kuitumika tena kwenye Ligi Kuu Soka ya Zanzibar. 
  Mwilo wa Jeba unatarajiwa kupumzishwa katika makaburi ya kijijini kwao Ndijani baada ya sala ya Adhuhuri. Mungu ampumzishe kwa amani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KIUNGO WA ZAMANI WA SIMBA SC NA AZAM FC IBRAHIM JEBA AFARIKI DUNIA KWAO ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top