• HABARI MPYA

  Alhamisi, Septemba 26, 2019

  NYOTA WA SIMBA SC ILIYOFIKA NUSU FAINALI KLABU BINGWA AFRIKA, ABBAS DILUBGA AFARIKI DUNIA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WINGA wa zamani klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam, Abbas Dilunga amefariki dunia usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake, Chanika, nje kidogo ya Jiji.
  Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Said Dilunga, mchezaji wa Ruvu Shooting ya Pwani, baba yake amefariki dunia ghafla tu nyumbani Chanika.
  “Ni kweli mzee ametutoka ghafla tu na msiba upo nyumbani kwake, Chanika”amesema Dilunga ambaye jana tu alikuwa kazini akiichezea Ruvu Shooting ikitoa sare ya 1-1 na Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  Abbas Dilunga (kushoto) akiwa na mwanawe, Said Dilunga ambaye anachezea Ruvu Shooting ya Pwani 
  Abbas Dilunga, wa tano kutoka kulia katika kikosi cha Simba SC kilichofika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974

  Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Said Dilunga, mchezaji wa Ruvu Shooting ya PwaniAbbas Dilunga ambaye enzi zake alipewa jina Kisungura kwa ujanja na mbio zake uwanjani, atakumbukwa zaidi kwa kuwemo kwenye kikosi tishio cha Simba SC miaka ya 1970 ambacho kiliweka rekodi mbalimbali katika medani ya soka.
  Mwaka 1974 walichukua Kombe la Afrika Mashariki na Kati Dar es Salaam na kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika kwa kuitoa Hearts Of Oak ya Ghana kabla ya kutolewa na Mehalla El Kubrasi. 
  Abbas ni mdogo wa mchezaji mwingine nyota kuwahi kutokea Tanzania, Maulid Dilunga (marehemu pia), ambaye enzi za uhai wake alichezea klabu ya Yanga.
  Maulid aliyefahamika kwa majina ya utani ya Eusebio na Mexico ndiye aliyeteuliwa kwenye kombaini ya Afrika kwa pamoja na kipa wa Simba SC, Omar Mahadhi Bin Jabir baada ya Fainali za Michezo ya Afrika (AAG) mwaka 1973 nchini Nigeria.
  Mwili wa marehemu Abbas Dilunga ambaye baada ya kustaafu soka alikuwa mganga wa tiba za jadi unatarajiwa kupumzishwa leo Saa 10.00 jioni, Kisarawe, mkoani Pwani. Mungu ampumzishe kwa amani marehemu Dilunga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NYOTA WA SIMBA SC ILIYOFIKA NUSU FAINALI KLABU BINGWA AFRIKA, ABBAS DILUBGA AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top